Gavana motoni kwa kuficha nakala za kuonyesha alivyotumia mabilioni
Na PETER MBURU
GAVANA wa Tana River Dhadho Godhana Jumatatu alikuwa na kibarua kigumu kujitetea mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti Kuhusu Uhasibu kuhusu ni kwa nini serikali yake ilikosa kumpa Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za serikali nyaraka za kuonyesha jinsi ilitumia pesa, mwaka wa 2017/18.
Ripoti ya Mkaguzi Mkuu Edward Ouko ilikosa kutoa maoni yoyote kuhusu jinsi gavana huyo alitumia pesa za mlipa ushuru, kwa kuwa maafisa wake hawakupewa nyaraka za kuonyesha jinsi pesa hizo zilitumika.
“Sina maoni kuhusu ikiwa pesa za umma zilitumika ipasavyo na kisheria jinsi katiba inasema kwa kuwa sikupata ushahidi wa kutosha kudhihirisha ama kuonyesha namna nyingine,” ripoti ya Bw Ouko ikasema.
Ripoti hiyo ilisema kuwa kaunti hiyo ilikosa kuzingatia utaratibu wa kuandaa bajeti, kwani haikuandaa nakala ya kuonyesha jinsi bajeti yake ilikuwa, haikuwa imewalipa wafanyakazi Sh101 milioni kufikia Juni 30, 2018 na kuwa maafisa wa serikali hiyo walitumia zaidi ya Sh40 milioni katika safari za nje ya nchi, japo hakukuwa na nakala za kuthibitisha.
Aidha, Bw Ouko alisema kuwa ijapokuwa kaunti hiyo iliripoti kuwa ilijitafutia Sh40 milioni, idara ya kukusanya ushuru kaunti hiyo iliweka Sh27 milioni pekee katika benki, wala hakuna pesa zilizohifadhiwa katika hazina ya CRF, kwa mujibu wa sheria.
“Mkaguzi anasema hajui lolote kuhusu jinsi ulitumia pesa za umma. Unawezakuwa mwanafunzi mzuri kama unavyojisifu kuwa umefanya kazi mashinani, lakini haja yetu ni matokeo. Tunatetea kaunti zipate pesa zaidi lakini sharti ziwajibike,” mwenyekiti wa kamati hiyo, seneta wa Homa Bay Moses Kajwang akasema.
Aidha, Mkaguzi Mkuu aliripoti kuwa kaunti hiyo haina rekodi kuhusu mali inazomiliki kwa sasa, madeni yake, wala mali ambazo ilipokea kutoka kwa usimamizi wa serikali za wilaya, za zamani.
Gavana Dhadho vilevile hakuthibitishia mkaguzi kuhusu matumizi ya Sh1.2 bilioni kununua mali ya serikali ya kaunti.