• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
NIPO SANA: City kumpokeza Pep mkataba mpya wa miaka mitano Etihad

NIPO SANA: City kumpokeza Pep mkataba mpya wa miaka mitano Etihad

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City atapokezwa fursa ya kuendelea kuhudumu uwanjani Etihad kwa miaka mitano zaidi.

Iwapo atakubali kurefusha kandarasi yake kambini mwa Man-City, kocha huyo mzaliwa wa Uhispania atakuwa akitia kapuni kima cha Sh2.8 bilioni mwishoni mwa kila mwaka.

Kufikia sasa, Guardiola angali na miaka miwili katika mkataba alionao na Man-City ambao waliweka historia msimu huu kwa kuwa kikosi cha kwanza cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutia kapuni jumla ya mataji matatu kwa mkupuo.

Mbali na kunyanyua ufalme wa taji la EPL, Man-City walitawazwa pia mabingwa wa Carabao Cup na Kombe la FA baada ya kuwachabanga Chelsea na Watford mtawalia.

Licha ya hofu kwamba huenda Man-City wakapigwa marufuku ya kushiriki kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kosa la kukiuka kanuni za usajili wa wachezaji (Uefa Financial Fair Play), Guardiola yupo radhi kutia saini makubaliano mapya na waajiri wake.

Kabla ya kuwaongoza Man-City kuchuana na Watford katika fainali ya Kombe la FA wikendi iliyopita, Guardiola mwenye umri wa miaka 48, alisisitiza kwamba hakuwa na azma yoyote ya kubanduka uwanjani Etihad mwishoni mwa msimu huu kwa nia ya kujiunga na Juventus.

Juventus kwa sasa wana ulazima wa kulijaza pengo la mkufunzi Massimiliano Allegri aliyeagana nao mwishoni mwa wiki jana baada ya kutimuliwa kwa kushindwa kuwatambisha waajiri wake katika kampeni za UEFA muhula huu.

“Ningependa sana kusalia hapa Man-City kwa misimu miwili zaidi. Hata hivyo, hilo litategemea iwapo bado watanihitaji. Ninaridhika sana kufanya kazi uwanjani Etihad na sioni sababu yoyote ya kunisukuma kutaka kwenda kokote kwingine,” akasema Guardiola.

Kipindi kirefu zaidi ambacho Guardiola amewahi kukamilisha kambini mwa kikosi kimoja ni miaka minne iliyomshuhudia akiwanoa miamba wa soka ya Uhispania, Barcelona. Baadaye, alipumzika kwa mwaka mmoja kabla ya maarifa yake kuwaniwa na Bayern Munich nchini Ujerumani. Alihudumu huku kwa kipindi cha miaka mitatu.

Msimu ujao utakuwa mwaka wake wan ne katika soka ya Uingereza na ni matarajio ya vinara wa Man-City kwamba Guardiola atarefusha muda wake kambini mwa kikosi hicho. Mipango ya Man-City ni kujishughulisha zaidi sokoni mwishoni mwa msimu huu na kusajili wanasoka wa haiba kubwa, japo kufanikiwa kwa hili kutategemea iwapo watakwepa shoka la Uefa.

Marufuku

Man-City huenda pia wakapigwa marufuku na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), EPL na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA); na hivyo kutoweza kushiriki biashara yoyote ya uhamisho wa wachezaji chipukizi.

Kulingana na Guardiola, Man-City wataingia katika kikoa cha miamba wa soka wenye majina ya kutajika zaidi duniani iwapo tu watatia kapuni ufalme wa taji la UEFA.

Baada ya kuwanyanyulia waajiri wake makombe matatu muhula huu, Guardiola kwa sasa analenga kutia kibindoni ubingwa wa taji la UEFA msimu ujao. Man-City wanajivunia kutia kibindoni mataji manne ya EPL, mawili ya FA na manne ya League Cup tangu umiliki wake utwaliwe na bwanyenye Sheikh Mansour mnamo 2008.

Kubwa zaidi ambalo Guardiola amesisitiza kwamba ni maazimio yake kambini mwa Man-City, ni kuwanyanyulia waajiri wake taji la UEFA chini ya kipindi cha miaka miwili ijayo.

Beki na nahodha Vincent Kompany, 33, amekuwapo kwa kipindi chote cha ufanisi huo wa Man-City.

Difenda huyo raia wa Ubelgiji anatarajiwa kuwa mchezaji na kocha wa kikosi cha Anderlecht, Ubelgiji msimu ujao.

You can share this post!

Uhuru apondwa Mlima Kenya

Bale katika hali tete ndani ya Real Madrid

adminleo