• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
Pep akiri Arsenal ni moto zaidi

Pep akiri Arsenal ni moto zaidi

NA MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City ameisifu klabu ya Arsenal kwa mwanzo mzuri baada ya timu hiyo kushinda mechi nane kati ya tisa.

“Kwa hakika tangu msimu uanze, Arsenal imekuwa na kikosi imara hata kuliko hata sisi msimu huu. Ushindi mfululizo katika mechi kubwa ni muhimu kwa timu yoyote inayotaka kushinda ubingwa wa ligi hii maarufu. Huu ni mwanzo mzuri kwa kocha Mikel Arteta, wakati huu timu nyingine kubwa zikiendelea kusuasua,” akasema Guardiola.

Arsenal majuzi walishangaza wengi baada ya kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya vigogo wa Liverpool, baada ya hapo awali kuandikisha ushindi wa 3-1 dhidi ya Tottenham Hotspur, na sasa wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 24.

Mabingwa watetezi Manchester City wanashikilia nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi moja, mbele ya Spurs walio na pointi 20, halafu Chelsea katika nafasi ya nne kwa pointi 16, lakini baada ya kucheza mechi chache.

Lakini akizungumzia madai hayo ya Guardiola, Arteta alisema atawaachia wadadisi kufanya uchambuzi, huku akisisitiza kwamba ni mapema mno kuanza kuzungumzia taji.

“Tunafurahia mahali tulipo kwa sasa, lakini hatujui mambo yatakavyokuwa baadaye,” akasema Arteta.

Kumekuwa na ulinganisho wa The Gunners na City, kufikia wakati huu ambapo timu hizo zimekuwa zikifuatana kwa karibu jedwalini.

Zote zimekuwa kwenye kiwango kizuri, huku City wakiendeleza rekodi ya kutoshindwa, wakati mshambuliaji wao tegemeo Haaland akiendelea kufunga mabao.

Guardiola anaamini kwamba Arsenal imekuwa bora zaidi msimu huu, huku akiongeza kwamba licha ya kikosi chake kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu, Arsenal imezua upinzani mkali katika kampeni za vijana wake kuwania kupigania ubingwa.

“Baada ya mechi tisa, tunafurahia kuendelea kubakia miongoni mwa mbili bora, wakati huu tunaendelea kuandikisha matokeo mazuri katika mechi za Klabu Bingwa barani Ulaya. Tumebakisha mechi moja tu kufuzu, lakini ni muhimu tumalize mechi zetu kwanza. Kuhusu EPL, tutasubiri kuona jinsi mambo yatakavyoenda.”

“Lakini hatutasahau ukweli kwamba, kuna timu moja ambayo inacheza vizuri kutuliko msimu huu. Huu ni ukweli mtupu. Kwa sasa hatuko kileleni, lakini ni vyema tupigane tuwe hapo haraka iwezekanavyo.”

Arteta alikuwa naibu wa Guardiola pale Etihad Stadium miaka ya hapo awali, kabla ya kuajiriwa na Arsenal baada ya Unai Emery kuondoka mnamo Desemba 2019.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Uamuzi wa Spika Wetang’ula kuhusu mrengo...

MITAMBO: Kifaa cha kukausha mazao kuwafaidi wakulima wadogo

T L