• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
WAKILISHA: Uchoraji pato na jukwaa kulea vipaji

WAKILISHA: Uchoraji pato na jukwaa kulea vipaji

Na PAULINE ONGAJI

ANAJIUNDIA kipato kupitia uchoraji, suala ambalo limemwezesha kukidhi mahitaji yake huku akiendelea na masomo chuoni.

Kutana na mchoraji shupavu, Brian Omwocha, 20, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kenyatta anakosomea masuala ya sanaa.

Omwocha ambaye kwa sasa anaendesha shughuli zake katika eneo la Ruiri, Nairobi, anasema kwamba kwa kawaida humchukua siku au hata wiki kadha kukamilisha mchoro mmoja huku ikitegemea na saizi, vile vile nyenzo zilizotumika.

Mojawapo ya kazi zake Brian Omwocha. Picha/ Hisani

Kwa kawaida michoro yake huwa kwenye turubai na ubao na hasa huhusisha mandhari ya kupendeza kwani anasema ni rahisi kuyatumia kuakisi jamii.

“Kila mchoro wangu unaakisi kitu fulani katika jamii,” aongeza.

Kufikia sasa amechora watu kadha ikiwa ni pamoja na Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Strathmore, Dkt Vincent Ogutu na mwanarepa Octopizzo.

Ni kazi ambayo imemsaidia kukidhi mahitaji yake ya kila siku na hata kusaidia familia yake.

“Kwa kawaida mimi huuza michoro yangu kwa kati ya Sh3,000 na Sh20,000 ambapo mara nyingi hutegemea na saizi ya turubai, vilevile malighafi mengine yaliyotumika,” aeleza huku akiongeza kwamba mwezi ukiwa mzuri anawezaunda hata Sh30,000.

Mbali na kumsaidia kifedha, kazi hii imemwezesha kukutana na watu wa ngazi tofauti katika jamii.

Licha ya faida hizi, bado anakumbwa na changamoto ya kupata fursa ya kuonyesha kazi zake.

“Jambo kuu ambalo limekuwa likichelewesha juhudi zangu za kuandaa maonyesho ya kazi zangu ni kwamba nimekuwa nikijihusisha na shughuli za kuchorea watu kazi zao, suala linalochukua muda wangu mwingi,” asema.

Safari yake katika fani ya uchoraji ilianza akiwa na umri mdogo huku ari yake ikichochewa na mchoraji aliyezuru nyumbani kwao.

“Nilikuwa na miaka tisa pekee ambapo kulikuwa na huyu mchoraji ambaye alikuwa amepewa kandarasi ndogo ya kuchora nyumbani kwetu. Baada ya kuona kazi yake safi, basi nikaamua kujaribu. Ni msukumo ambao ulizidishwa na motisha kutoka kwa wazazi na ndugu zangu,” aeleza.

Mbali na kuchora ili kujipa kipato, Januari mwaka huu akiwa na mwenzake Rickton Kariuki, walianzisha mradi kwa jina Tusijimade Wasanii kusaidia kukuza vipaji vya wasanii.

“Nia yetu ni kusaidia wasanii kutoka nyanja mbalimbali za sanaa kama vile uigizaji, uimbaji na uchoraji ambapo kupitia mtandao sote tinajifunza jinsi ya kupiga msasa vipaji vyetu,” aeleza.

Kupunguza visa vya uhalifu

Kwa kufanya hivi, asema, watakuwa wanapunguza visa vya uhalifu.

“Tayari tumeanza kushuhudia matokeo kwani kumekuwa na vijana ambao awali walikuwa wakijihusisha na uhalifu, lakini sasa wamejitokeza wakitaka kujiunga na mradi huu na hivyo kujitafutia riziki,” aeleza.

Ari yao ya kuanzisha mradi huu ilitokana na ongezeko la visa vya mauaji ya vijana kwa sababu ya uhalifu.

“Niligundua kwamba vijana wengi ambao walikuwa wakiuawa na polisi kwa sababu ya uhalifu, walikuwa na vipaji vya hali ya juu. Kwa mfano kuna rafiki yangu mmoja alipigwa risasi na kufariki, na katika harakati hizo kipaji chake cha uimbaji kikatokomea. Pia, kuna rafiki yangu mwingine aliyekamatwa na polisi na kufungwa gerezani,” aeleza.

Anasema kwamba ndoto yake ni wakati mmoja kuungana na wachoraji wengine wa kimataifa na kuonyesha kazi zake katika makavazi maarufu ya Louvre Museum, jijini Paris, Ufaransa.

Aidha, wakati mmoja anatumai kusaidia wachoraji kama yeye kwa kufungua studio ya kuonyesha kazi zake.

“Kwa upande mwingine, ndoto yetu ni kujitosa katika sanaa ya thieta kurekodi filamu fupifupi tukitumai kupata washirika zaidi watakaotupa mfichuo katika ngazi za kimataifa,” aongeza.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Simpendi wala sina hisia kwake ila ataka...

MAPOZI: Nick Mutuma

adminleo