Habari Mseto

Wakenya waliodhulumiwa na serikali wajitokeze – LSK

February 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Rais wa Chama cha Wanasheria nchini Bw Isaac Okero. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha Wanasheria nchini (LSK) kimewataka Wakenya kuwasilisha taarifa kuhusiana na amri za mahakama kote nchini ambazo zimepuuzwa na serikali.

LSK pia imewataka wananchi waliodhulumiwa haki kugandamizwa na serikali wajitokeze na kuwasilisha malalamishi yao kwa chama hicho.

“Tunahimiza wananchi kuwasilisha ripoti kuhusiana na amri za mahakama zilizopuuzwa na idara au maafisa wa serikali,” ikasema LSK.

“Malalamishi hayo yatawasilishwa katika Afisi ya Rais, Jaji Mkuu na Maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti,” ikaongezea.

Alhamisi iliyopita, wanasheria waliandamana jijini Nairobi kupinga hatua ya serikali kupuuza msururu wa maagizo yanayotolewa na mahakama.

Miongoni mwa maagizo yaliyopuuzwa na serikali ni lile lililotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Luka Kimaru aliyetaka mwanaharakati wa NASA Miguna Miguna aachiliwe huru kwa dhamana lakini serikali ikakataa kufanya hivyo na badala yake ikamsafirisha nchini Canada.

“Serikali haiwezi kupuuza maagizo yanayotolewa na mahakama. Kwa sababu kwa kufanya hivyo kila Mkenya atapuuza na utawala wa sheria na mahakama zitatoweka,” akasema Rais wa LSK Isaac Okero.