Kombora nililopiga Leicester ni leseni ya kuondoka Etihad – Kompany
NA CECIL ODONGO
NAHODHA wa Manchester City Vincent Kompany amefichua kwamba aliamua kubanduka kambini mwa timu hiyo alipofunga bao kupitia kiki ya mbali kwenye mechi dhidi ya Leicester City mnamo Mei 6.
Bao hilo lililofungwa dakika ya 70 lilisaidia vijana wa kocha Pep Guardiola kuwashinda the Foxes 1-0 ugani Etihad na kuipiku Liverpool kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) .
“Nilipofunga bao hilo nilifahamu kwamba muda wangu katika timu ya Manchester City ulikuwa umekamilika. Singeweza kufanya mengine ya ziada na bao lilipoingia niliridhika kwamba nimeweza kutimiza malengo yangu Etihad,” akasema
Mbelgiji huyo vile vile alisema kwamba hasikitishwi na jitihada za Manchester City kushinda Klabu Bingwa Barani Ulaya (Uefa) kuambulia pakavu msimu huu wa 2018/19 akisema bado wana nafasi ya kushinda taji hilo msimu wa 2019/20.
“Kulingana nami, Mancity ndiye klabu bora zaidi duniani. Haijalishi iwapo walishinda Uefa au la kwa sababu ni klabu kubwa ambayo inazidi kuimarika kwa kasi,” akaongeza Kompany.
Jumapili Mei 19, mlinzi huyo matata alitangaza kwamba atajiunga na klabu yake ya utotoni ya Anderlecht kama mchezaji na mkufunzi.