Habari Mseto

Mfumo wa dijitali waisaidia Co-op kuvuna faida ya Sh3.5b kwa miezi mitatu

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Co-operative Kenya, imepata faida ya asilimia 4.4 katika robo ya kwanza ya mwaka wa kifedha kufikia Machi.

Faida hiyo ilitokana na ongezeko la mapato kutokana na mikopo na mapato ambayo hayajafadhiliwa na gharama ya chini ya operesheni.

Mapato ya benki hiyo katika muda huo yalikuwa ni Sh3.59 bilioni ikilinganishwa na Sh3.44 bilioni mwaka uliotangulia.

Mapato kutokana na riba ya dhamana za serikali yaliongezeka kwa asilimia 39.6 hadi Sh2.8 bilioni katika kipindi hicho kutokana na ongezeko la mikopo kwa serikali kwa asilimia 38.6 hadi Sh103.9 bilioni kutoka Sh75 bilioni kipindi hicho mwaka uliotangulia.

Kuimarika kwa mapato ya benki hiyo pia kulisaidiwa na ongezeko la asilimia 19.1 kwa mapato yasiyo riba, ambayo yaliongezeka hadi Sh4.2 bilioni.

Gharama ya utekelezaji wa operesheni ilipungua kwa asilimia 1.2 hadi Sh6 bilioni katika kipindi hicho.

Afisa Mkuu Mkurugenzi Gideon Muriuki alisema usimamizi mwema wa gharama, upanuzi wa njia za kujipa pato na utekelezaji shwari wa operesheni ulisaidia benki hiyo kupata faida ya juu.

“Mfumo dijitali hasa M-Co-op ulisaidia sana kuimarisha pato lisilotokana na riba kutokana na kuwa wateja 4.3 wamejisajili na mikopo 1.2 milioni ya thamani ya Sh5.1 bilioni na zaidi kutolewa,” alisema Bw Muriuki.

Kulingana na benki hiyo, imetoa operesheni zake nje kwa asilimia 88, ambapo biashara kubwa zaidi hutekelezwa na wateja wake kupitia kwa kiosk za kujihudumia, matawi 155 na maajenti 11,600.