Mwanamume ataliki mkewe ili aishi na mamaye mzazi
Na PETER MBURU
MWANAMUME ameamua kuishi na mamaye mzazi badala ya mkewe, hali ambayo imeifanya mahakama moja ya Nairobi kuvunja ndoa baina yao.
Katika kesi hiyo ya talaka, mwanamke husika alimpa mumewe chaguo, aidha aishi naye ama na mamake, ila hawangeishi nyumba moja wakiwa watatu, nyumbani kwao mtaani Lang’ata, Jijini Nairobi.
Hata hivyo, chaguo la mwanamume huyo lilikuwa la kipekee, akiamua kuishi na mamake.
Ndoa ya Hussein na mkewe Dayman haijakuwa na matatizo makubwa kama ya ukosefu wa uaminifu, kuteswa ama kutelekezwa kama jinsi hali imekuwa katika kesi zingine za talaka, lakini kisa hicho kimesababisha talaka ya wanandoa hao.
Mzozo ulikuwa kuwa, mkewe Hussein alimtaka mavyaa wake kuondoka nyumbani kwao na madai kuwa alikuwa akikataa kunyonyesha mtoto wao vyema, kesi ambayo Kadhi alisema ingesuluhishwa hata nje ya korti.
Mwanamke huyo ndiye aliwasilisha kesi hiyo akitaka talaka Januari na korti ikawapa chaguo la kutafuta mzee awasuluhishie mizozo baina yao.
Lakini hilo halikuwezekana, kwani wote walirejea mahakamani wakitaka kutenganishwa.
Wawili hao walioana Novemba 2015 na wamejaliwa na watoto wawili; wa miaka miwili na mwingine mchanga.
Malalamiko ya pekee kutoka kwa mwanamke huyo yalikuwa kuwa mavyaa wake alifika nyumbani kwao na kuanza kuwatawala, akimfanya kukaa kama kijakazi.
Alimtaja mumewe kuwa mlegevu, akisema alishindwa kuwapatanisha na mamake, kusuluhisha mzozo kuhusu utawala wa boma lao.
Aidha, alimlaumu mumewe kuwa hakuthibiti usiri wa ndoa, akisema nyumbani kwao kulikuwa kumejaa watu wa familia yake.
Hussein alieleza korti kuwa mkewe huyo alitoroka kutoka nyumbani kwao Oktoba 2017, walipokuwa wamempeleka mtoto wao wa miaka miwili hospitalini, kwa utapia mlo.
“Dayman hakuwa wa kuwajibika kwani alimsababishia mtoto utapia mlo,” akasema.
Rekodi za korti aidha zilionyesha kuwa wawili hao walipofika kortini walikataa kupatanishwa.
“Wote walipigania kutenganishwa na ndoa yao kuvunjwa, japo kutokana na masuala ambayo yangeweza kusuluhishwa nje ya korti. Hussein alikuwa katika kibarua cha kuchagua ikiwa aishi na mkewe ama mamake na akaamua kuishi na mama. Huenda kutenganishwa kwa mamake na mkewe kungeokoa ndoa yao,” akasema Kadhi Mkuu, Sebastian Ratori.