Ripoti yafichua 'serikali mbili' Kenya
Na LEONARD ONYANGO
KENYA inatawaliwa na serikali mbili – moja iliyochaguliwa na wananchi na nyingine ya wakora wenye uwezo mkubwa wa kifedha na kibiashara.
Kulingana na ripoti iliyotolewa Jumatano, “serikali ya wakora” inajumuisha wanasiasa, matapeli na wafanyibiashara, ambao wamepenyeza nguvu zao kwenye wizara, mashirika na taasisi nyingine za serikali, polisi, Idara ya Mahakama na sekta ya kibinafsi.
“Magenge haya ya uhalifu yameteka nyara serikali na yanaendeleza shughuli zao kwa kujificha kwenye Katiba,” ripoti hiyo ya shirika la AfriCog inaeleza.
Kulingana na ripoti hiyo, wanasiasa wa Serikali na wale wa upinzani ni washirika wakubwa katika kuiba mali ya umma na wengi wao huchaguliwa wakiwa na nia ya kujitajirisha kibinafsi wala sio kusaidia wananchi.
Ni kutokana na “serikali ya wakora” ambapo juhudi za Rais Uhuru Kenyatta za kupambana na ufisadi zimeshindwa kuzaa matunda, inasema ripoti hiyo.
“Serikali ya wakora inajumuisha kundi la wachache wenye mamlaka na utajiri mkubwa. Wamepunguza nguvu za taasisi za serikali katika kuhakikisha sheria inafuatwa, wamefanya utekelezaji wa sheria kufanywa kwa ubaguzi, mashirika ya umma yananyanyaswa, chaguzi huru zinavurugwa na wale wanaoshinda ni wanaotumia fujo na ufisadi zaidi,” yaeleza ripoti hiyo.
Inaeleza kuwa ni kutokana na “serikali ya wakora” ambapo kashfa kubwa kubwa za ufisadi kama Goldenberg, Anglo Leasing na Eurobond zimekosa kutatuliwa.
“Kesi zinazohusisha sakata kubwa za ufisadi hazijawahi kutatuliwa. Wahusika ambao wanahusisha viongozi wa serikali, wanasiasa wa upinzani na wafanyabiashara maarufu hawataki kesi hizo kuchunguzwa kwa sababu wanahofia kuwa watafichuliwa,” akasema Bw Wachira Maina, wakili wa masuala ya kikatiba ambaye ni miongoni mwa waandalizi wa ripoti hiyo.
Ripoti inasema “serikali ya wakora” inadhibiti taasisi zote zinazofaa kudumisha demokrasia kama vile Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Polisi kati ya asasi nyinginezo.
“Watu hao wenye ushawishi mkubwa huhakikisha kuwa taasisi hizo zimekuwa duni na huwanunua wanasiasa ili kuwaunga mkono,” inasema ripoti hiyo iliyozinduliwa jijini Nairobi katika hafla iliyohudhuriwa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, Mwanauchumi David Ndii, Mkurugenzi wa Inuka Kenya John Githongo kati ya wanaharakati wengine.
Ripoti hiyo pia imekosoa jinsi Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wamekuwa wakiendesha vita dhidi ya ufisadi.
Kwa mujibu wa ripoti, operesheni inayoendelea nchini dhidi ya wafisadi inachochewa na sababu za kisiasa.
“Operesheni inayoendelea dhidi ya ufisadi inaongozwa na masilahi ya kisiasa na ndiyo maana afisi ya DPP inashindwa kutetea kesi mahakamani,” inasema ripoti.
Shirika la AfriCog pia limeshutumu serikali kwa kupuuza ripoti za chunguzi zinazotolewa na kamati za bunge zikipendekeza maafisa fulani serikalini wachunguzwe kwa kuhusika katika ufisadi.
Ripoti hiyo inatoa mfano wa sakata ambapo makamishna wa IEBC walidaiwa kupokea hongo wakati wa kutoa kandarasi kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2013.
“Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC) ilipendekeza makamishna wote wa IEBC wachunguzwe na wazuiliwe kushikilia afisi za umma kwa kutoa kandarasi tatanishi ya Sh258 milioni. Hakuna pendekezo hata moja lililotekelezwa. Badala yake walimwondoa mkurugenzi wa tume James Oswago na nafasi yake ikachukuliwa na Bw Ezra Chiloba,” inasema ripoti.
“Katika uchaguzi wa 2017, tume ya EACC ilipendekeza jumla ya wawaniaji 106 wazuiliwe kugombea kwa kukiuka maadili. Lakini tume ya IEBC ilipuuza mapendekezo hayo na kuwaruhusu kuwania na 60 kati yao walishinda viti,” inaongezea.