Ripoti yafafanua Uhuru hatafaulu kumaliza ufisadi
Na LEONARD ONYANGO
AHADI za Rais Uhuru Kenyatta kwa Wakenya kila mara kuwa hatalegeza kamba kwenye vita dhidi ya ufisadi zitabakia kuwa ndoto, ripoti ya AfriCOG ilieleza Jumatano.
Hii ni licha ya Rais Kenyatta hapo jana kuapa kwa mara nyingine kuwa amejitolea kuhakikisha amemaliza ufisadi nchini.
Kulingana na AfriCOG, juhudi za Rais Kenyatta zinapaswa kuungwa mkono, lakini hazitafaulu kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya ufisadi na siasa.
Ripoti ya AfriCOG iliyotolewa jana inasema kundi ndogo la matajiri wakubwa na wenye mamlaka serikalini limeteka serikali kuu na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuiba mali ya umma.
“Lengo kuu ni kuiba kiasi kitengeza kiasi kikubwa cha fedha kwa matumizi kwenye kampeni ili kuendelea kushikilia madaraka na kujitajirisha zaidi,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa “serikali ya wakora” iko na nguvu nyingi za kifedha na madaraka pamoja na kupenyeza katika taasisi za polisi, Idara ya Mahakama na sekta ya kibinafsi, hivi kwamba linavuruga juhudi zozote za kukabiliana na ufisadi hata kama zinaongozwa na Rais Kenyatta mwenyewe.
Kutokana na hali hii, inasema, vita dhidi ya ufisadi havitafanikiwa kwani vinavurugwa na maajenti wa “serikali ya wakora” katika idara za uchunguzi, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na mahakamani.
Ripoti hiyo inasema “serikali ya wakora” imezima kabisa nguvu za wananchi kupata haki ama kuchagua watu wanaoweza kuwakomboa kutokana na umaskini, kwa kuhakikisha wanaochaguliwa hasa katika vyeo vya juu ni watu watakaotekeleza ajenda zake.
“Mbinu inayotumika na ‘serikali ya wakora’ katika kuhakikisha wananchi hawana usemi ni kubadilisha miundo ya siasa katika kila uchaguzi, ili kuhakikisha wanaoingia serikalini wanazingatia maslahi yake na wala sio ya wananchi,” yasema ripoti hiyo.
Mwaka jana Rais Kenyatta alitangaza vita vya kupambana na ufisadi. Kati ya juhudi alizotekeleza ni kufanyia mabadiliko taasisi za Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Mwaka jana maafisa wa ngazi za juu serikalini walikamatwa na kushtakiwa na kesi kadhaa zinaendelea mahakamani.
DCI pia inaendelea na uchunguzi kuhusu madai ya ufujaji wa mabilioni ya pesa za miradi ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer, lakini kufikia sasa hakuna washukiwa walioshtakiwa.