Jombi atemwa kwa kukataa kuchovya asali
Na LEAH MAKENA
HANANTU, THARAKA NITHI
JAMAA wa hapa alitemwa na demu wake kwa kukataa kuchovya asali akisema hangejihusisha na tendo la ndoa kabla ya harusi.
Kidosho na polo walikuwa kwenye uhusiano kwa muda wa miaka miwili na baada ya kuelewana wakajifahamisha kwa wazazi na marafiki huku mipango ya harusi iking’oa nanga.
Hivi majuzi, kidosho alishangaza wengi alipotaka mipango yote ya harusi kusitisishwa akidai alikuwa na swala muhimu alilotaka kujadili kabla ya mipango kuendelea.
Alipotakiwa kujieleza, mwanadada alipasua mbarika na kusema kuwa hakuwa tayari kuingia kwenye ndoa na mume ambaye hakumfahamu vizuri.
“Tumechumbiana kwa zaidi ya miaka miwili sasa ila hili dume linanishangaza kwa kukataa kata kata kukagua katiba likidai linataka tufunge ndoa kwanza. Nina hofu ya kufunga pingu za maisha na shoka ambalo halikati na hivyo siwezi kujiweka hatarini”, kidosho alikiri.
Akina mama waliofanyia binti kikao walipopata tetezi zake na kumtaka kushukuru Mungu kwa kupata mwanaume mwaminifu.
“Haufai kulalamika au kukosoa msimamo wa mchumba wako. Unafaa kushukuru Mungu kwa kukupatia mwanamume mwaminifu anayejiheshimu,” mama mmoja alimweleza mwanadada.
Hata hivyo, mrembo alipinga mawazo yao na hakuna aliyefanikiwa kumshawishi kuendelea na mipango ya harusi.
“Hapana, ninashuku huyo jamaa ana dosari fulani. Hata kunigusa pekee hajawahi kwa miaka yote ambayo tumekuwa wachumba. Sitaki kujitumbukiza kwenye shida. Heri nijitoe mapema,” alisema.
Kwa upande wake, polo alishikilia msimamo wake na baada ya wawili hao kushindwa kuelewana kuhusu suala hilo wakalazimika kutupilia mbali penzi lao.