WANDERI: Wakenya sasa wafaa kukasirika kwa maovu
Na WANDERI KAMAU
SAKATA ya dhahabu ghushi ni kashfa ‘hewa’ ambayo itapotea na kusahaulika kabisa. Ni moto ambao utawaka na kuzima.
Baadaye, kama ilivyo katika Kenya na nchi zingine, wimbi lingine litaibuka na kusahaulika. Huu ndio mtindo wa hapa Kenya.
Nchini Kenya, baadhi ya sakata kubwa zaidi ambazo zimelikumba taifa hili ni Goldenberg, Anglo-Leasing, Eurobond, Shirika la Kitaifa kwa Huduma za Vijana (NYS) kati ya zingine.
Katika sakata hizi zote, mabilioni ya pesa yamepotea. Hata hivyo, Wakenya hawajawahi kuonyesha ghadhabu yoyote inayoweza kushinikiza mageuzi au wale wanaotuhumiwa kuhusika kuwajibika.
Katika sakata hii ya dhahabu, inakisiwa kuwa dhahabu inayodaiwa kuzuiliwa Kenya ni ya thamani ya Sh30 bilioni.
Sikitiko zaidi ni kuwa mzozo huu sasa unatishia uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Muungano wa Milki ya Kiarabu (UAE).
Bila shaka, mvutano huu huenda ukahatarisha maisha ya maelfu ya Wakenya wanaofanya kazi mbalimbali katika nchi za Uarabu.
Ni sakata ambayo pia inadhihirisha kuwa Kenya ni kitovu cha mitandao ya ulanguzi wa bidhaa mbalimbali.
Kinaya kikuu ni kwamba, Kenya ni mwanachama wa mikataba ya Umoja wa Mataifa (UN) kukabili biashara za magendo.
Mbali na hayo, sakata hii inaashiria kudorora kwa maadili ya viongozi wa kisiasa, kwani wao ndio wahusika wakuu.
Katika sakata ya Goldenberg, hakuna mshukiwa hata mmoja ambaye alihukumiwa, licha ya majina yao kufichuliwa na kuibuka kwamba waliipora Kenya zaidi ya Sh13.6 bilioni! Je, ni lini Wakenya watazinduka?
Utathmini wa kina wa asili ya maasi yaliyoibuka katika nchi za Kiarabu mnamo 2011, unadhihirisha wazi kuwa yalisababishwa na hasira ya raia kutokana na kutowajibika kwa viongozi wao.
Maasi hayo yalianzia nchini Tunisia na kusambaa katika nchi zingine kama Libya, Misri na Yemen.
Hilo lilisababisha kung’atuliwa mamlakani kwa marais Idine Ben Ali wa Tunisia, Hosni Mubarak wa Misri, Ali Saleh wa Yemen na aliyekuwa kiongozi wa mrefu wa Libya, Muammar Gaddafi.
Majuzi, maasi hayo pia yalitua nchini Sudan, ambayo pia asilimia kubwa ya raia wake ni Waarabu, na kusababisha kung’atuliwa wa aliyekuwa kiongozi wake, Hassan el Bashir.
Kiini cha maasi ya Sudan ni kupanda kwa bei ya mkate. Hiyo ndiyo ilikuwa chemichemi ya maandamano hayo, yaliyoanzia katika jiji la Omdurman.
Cha kushtua ni kwamba katika mwisho wa maandamano hayo, wanajeshi ambao walikuwa wakimuunga mkono Bashir walimgeuka!
Katika kitabu The Wretched of the Earth, mwandishi Frantz Fannon anaeleza jinsi wananchi wanaweza kutumia nguvu zao kujikomboa.
Inawezekana Kenya? Je, sakata hizi zitakuwa wingu lipitalo tu bila hatua na ghadhabu kutoka kwa wananchi?