• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
AKILIMALI: Amebuni ajira kwa vijana wenzake kwa kuanzisha kituo cha runinga

AKILIMALI: Amebuni ajira kwa vijana wenzake kwa kuanzisha kituo cha runinga

Na FRANCIS MUREITHI

HUKU serikali za kaunti zikifurahia matunda ya ugatuzi, kijana mwenye uchu wa kufanya biashara, amebadilisha ajenda 14 za ugatuzi ambazo zinatekelezwa mashinani kujipatia riziki.

Aidha, kijana huyu barubaru amegeuza ajenda hizo kuwa mfereji wa kujipatia donge nono kwa kupeperusha habari moja kwa moja kupitia televisheni ya mtandaoni.

Na ikiwa hamu ya kutumia huduma zake ni kigezo cha kupima jinsi wakazi wa Nakuru wanavutiwa na televisheni hii al maarufu Nakuru TV, basi bila shaka mwekezaji huyu chipukizi anajiwekea kibindoni kitita kizuri cha hela katika kaunti inayokisiwa kuwa na zaidi ya wakazi milioni mbili.

“Kazi hii ina pesa kwani katika miezi mitatu ya kwanza nilipata faida ya Sh100,000 hata kabla sijanunua vifaa zaidi vya kisasa kuimarisha upeperushaji wa habari,” anasema Bw Patrick Kinyua Maina ambaye ndiye mwanzilishi wa Nakuru TV.

“Mwaka wa kwanza mapato yangu ya jumla yalikuwa Sh500,000 na matumaini yangu ni kugonga Sh1 milioni hivi karibuni na kuongeza idadi ya watazamaji,” anasema Bw Kinyua.

Bw Kinyua huwatoza wateja wake kati ya Sh15,000 hadi Sh40,000 kupeperusha matangazo moja kwa moja kwa kati ya muda wa saa mbili na saa tatu na hutegemea kama ni wateja wa kawaida au kampuni.

Hata hivyo, vijana wanaoendeleza talanta zao ada zao huwa ni za afueni kwani nia yake ni kupanua talanta hizo katika kaunti.

Televisheni hii ya mtandao ambayo ilianzishwa miaka miwili iliyopita, inazipa kipaumbele habari za mashinani na hivyo kuwa tegemeo la wengi wanaofuatilia kwa karibu matumizi ya mabilioni ya pesa za ugatuzi.

Kutokana na umaarufu wake unaozidi kuongezeka kila kuchao, habari za kituo hiki zimekuwa kwenye vinywa vya wakazi wengi kwenye hafla nyingi na gumzo mitaani huku wakipigia kituo hiki debe kwa kuwapa habari motomoto.

Kituo hiki ambacho makao yake makuu yako katika jengo la Highway Towers katikati mwa mji wa Nakuru orofa ya saba, lina wateja kutoka ndani na nje ya nchi.

Shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani Deutsche Welle ni miongoni mwa mashirika ya kimataifa yanayodandia huduma za televisheni hii na Wakenya walioko mataifa ya ng’ambo wanaotaka kujumuika na jamii zao humu nchini kufanya mikutano ya faragha kama vile kulipa mahari na sherehe za harusi miongoni mwa mikusanyiko mingine ya kijamii.

Nakuru TV inatoa huduma zake pembe zote za kaunti ya Nakuru kupitia mtandao katika kompyuta.

Wakazi wa Nakuru sasa wanapata habari za michezo, siasa, biashara, afya, miongoni mwa habari nyingine al mradi tu wako na simu za mkononi, kompyuta ndogo aina za laptops au tablets mahali popote walipo katika kaunti.

Bw Kinyua, ambaye ndio mwanzo umri wake unagonga miaka 30, amewezesha wakazi kuelewa na kufafanua kwa ufasaha masuala ya ugatuzi.

Anajuilikana sana kama “Prince” miongoni mwa wanahabari mjini Nakuru na anadokeza kuwa Nakuru TV inalenga kubadilisha mawazo ya wakazi na kuwapa changamoto wakazi umuhimu wa kufuatilia kwa karibu maendeleo na matumizi ya pesa za umma katika kaunti.

Wazo la kuanzisha kituo hiki lilimjia kama vile mawazo mazuri humjia mtu akiwa kwenye bafu akioga.

“Ndoto yangu ni kuhakikisha ajenda 14 za ugatuzi ambazo kulingana na katiba ni sharti zitekelezwe mashinani zinatimizwa na serikali ya kaunti ya Nakuru kwa kufuatilia karibu matumizi ya pesa na kuwahamasisha wakazi umuhimu wa kushiriki mikutano ya bajeti,” anadokeza Bw Kinyua.

“Mimi ni mwandishi wa habari wa redio na natumia mafunzo niliyopata kuwapa watazamaji wa Nakuru TV habari ambazo zitabadilisha hali yao ya maisha mbali na kuwapa habari za burudani na za kumtukuza Maulana,” anasema.

Bw Kinyua anafichua kuwa umaarufu wa Nakuru TV unazidi kuimarika kwani vituo vikuu nchini huzipa habari na ugatuzi mashinani muda mfupi sana.

“Habari tunazozipa umuhimu zinawahusu wakazi wa kawaida, wachuuzi, wafanyabiashara wadogo, michezo, siasa, maendeleo, dondoo za hapa na pale mitaani miongoni mwa habari nyingine za kusisimua,” anasema Bw Kinyua.

Ununuaji vifaa

Asema alitumia akiba ya Sh70,000 kuanzisha Nakuru TV kwa kununua vifaa vya kisasa kutoka Marekani kutimiza ndoto yake.

“Nilianza kwa kununua kifaa cha kisasa cha kompyuta ndogo (laptop) na bado naongeza vifaa zaidi kuimarisha kituo hiki,” anasema Bw Kinyua.

Kufikia sasa anakadiria kuwa vifaa vyote alivyonunua ni vya thamani ya zaidi ya Sh500,000.

Licha ya kuwa hajaanza kupata faida nono, Bw Kinyua anasema kuwa kituo hiki kinampa riziki na posho yake ya kila siku bila kunung’unika kwa kuwa anatimiza mahitaji yake mengi maishani.

Bw Kinyua anasema anakerwa kila anapowaona vijana waliohitimu kwa shahada za uandishi wa habari kutoka vyuo vikuu wakitumia muda wao mwingi kwenye mitandaoa kutazama sinema na video chafu za mapenzi.

“Wosia wangu kwa vijana wanaotangatanga mitandaoni wakitafuta mapenzi feki ni watumie maarifa na elimu waliyopata kuanzisha kampuni za kibiashara mitandaoni na kujipatia riziki ili kuongeza nafasi za kazi miongoni mwa vijana wenzao wanaosubiri kazi nadra za ofisi,” anasema Bw Kinyua.

Alipoanzisha kituo hiki alimwajiri mfanyakazi mmoja lakini sasa amewaajiri wafanyakazi tisa miongoni mwao kutoka vyuo vikuu vya humu nchini.

You can share this post!

ONYANGO: Wananchi washinikize magavana kutekeleza manifesto...

Afisi mpya ya ardhi yafunguliwa mjini Ruiru

adminleo