• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
AKILIMALI: Gharama ya kilimo cha uzalishaji mananasi ni ya chini, mapato ni bora

AKILIMALI: Gharama ya kilimo cha uzalishaji mananasi ni ya chini, mapato ni bora

Na SAMMY WAWERU

NI maeneo machache yanayojulikana kuzalisha mananasi nchini nayo ni Thika, Malindi, Kisii na Kericho.

Maeneo kadha Magharibi mwa Kenya, Nandi na pia Gatundu, nako pia kunakuzwa matunda haya.

Aidha, matunda haya yalizalishwa mara ya kwanza Amerika Kusini, lakini sasa yameenea mataifa mengine ulimwenguni.

Sehemu zinazoyanawirisha ni zenye urefu wa kati ya mita 100 hadi mita 1800, juu ya ufuo wa bahari (altitude) na yanayopokea kiwango cha mvua kati ya milimita 600 hadi 3,800 kwa mwaka.

Hata ingawa mananasi yanahitaji wastani wa mvua milimita 1100 kwa mwaka, wataalamu wa masuala ya kilimo wanafafamua pia yanastawi maeneo yanayopokea wastani wa milimita 750.

Pia hulimwa kupitia mfumo wa kunyunyizia mashamba maji kwa mifereji (Irrigation). Kiwango cha joto, kinapaswa kuwa nyuzijoto 18-45 sentigredi.

Kulingana na Bw James Kimemia, mtaalamu wa kilimo Murang’a, matunda haya yanahitaji udongo usiotuamisha maji kama vile tifutifu na kichanga.

“Mananasi hayastawi katika udongo unaotuamisha maji au chemichemi. Mkulima aepuke udongo mweusi wa kufinyanga kwani hutuamisha maji,” anashauri Bw Kimemia.

Kiwango cha asidi ya udongo (pH) kiwe kati ya 4-5, kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyu.

Mananasi ni matunda matamu yaliyosheheni sukari, ambayo ni hai. Pia ni kiini kizuri cha Vitamini A na C.

Mbali na faida zake kiafya, matunda haya yana tija chungu nzima kimapato kwa anayekumbatia kilimo chake. Yakilinganishwa na matunda mengine, hayana ugumu kuyakuza.

Kulingana na Bi Teresiah Waceke, anayeyapanda Gatundu Kusini, kaunti ya Kiambu, kazi huwa kuandaa shamba pekee. Yanapopandwa, mkulima huhitaji kupalilia minanasi ili kuondoa makwekwe. “Ukiwa na chanzo cha maji ya kutosha, kazi ni kuandaa shamba, kupanda na palizi. Kifuatacho ni mavuno yakutuze,” anasema mkulima huyu.

Waceke huyakuza katika shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari tano.

Matayarisho na taratibu za upanzi

Kulingana na James Kimemia, mtaalamu wa kilimo, maandalizi duni ya shamba la kupanda mananasi hushusha kiwango cha mazao na hata hadhi yake.

Anahimiza maandalizi kuwa kabambe, ambapo shamba linapaswa kuchimbwa karibu futi tatu kuenda chini.

Shamba lipewe muda wa kati ya wiki mbili hadi nne, makwekwe yakauke.

Mashimo ndiyo bora kupanda minanasi, na yanafaa kuwa na urefu wa futi mbili hivi kuenda chini.

“Nafasi kutoka shimo moja hadi lingine huandaa futi tatu, kwa sababu mananasi huzalisha matawi mengi,” anaelezea Bi Waceke.

Udongo uliotolewa kwenye mashimo huchanganywa na mbolea, halafu mchanganyiko huo unarejeshwa shimoni. Mbolea ya mifugo ndiyo bora katika ukuzaji wa matunda.

Mbegu za matunda haya ni matawi ya liyopogolewa (suckers), na ndiyo hupandwa. “Minanasi inapaswa kupogolewa ili kuzalisha matunda makubwa na bora. Matawi yakiwa mengi, huwa ya hadhi ya chini na madogo kwa sababu hung’ang’ania lishe ambayo ni mbola na maji,” afafanua Bw Kimemia.

Iwapo unataka kulima mananasi kwa mara ya kwanza, mbegu zake utazipata kutoka kwa wakulima wa matunda haya. Tawi hugharimu Sh10, au kulingana na maafikiano kati yako na muuzaji.

Maeneo yasiyopokea mvua ya kutosha kufanikisha kilimo chake, mfumo wa kunyunyizia mimea maji hutumika na aghalabu huyalisha maji mara tatu kwa wiki. Palizi hufanywa makwekwe yanapomea, na unahimizwa kuwa makini wakati wa shughuli hiyo.

Wataalamu wa kilimo wanasema mananasi hunawirishwa zaidi yanapotiwa mbolea iliyosheheni madini ya Nitrojini (top dressing), miezi sita baada ya upanzi.

Changamoto ni haba

Matunda haya ni nadra kushambuliwa na wadudu ikiwa mkulima atazingatia taratibu bora kitaalamu.

Wadudu wanaoshuhudiwa japo ni mithili kutaka kutazama kivuli cha nchi ni Nematode na Vithiripi.

Pineapple top na root rot, white leaf spot, yellow spot virus, na pineapple wilt virus ni baadhi tu ya magonjwa yanayoathiri mananasi.

Fuko ndio kero kuu katika kilimo cha mananasi.

Wanyama hawa hufukua mizizi ya minanasi na kufanya ikauke.

Hudhibitiwa kwa kutumia mitego maalumu ya kuwanasa.

Matunda haya hukua kati ya miezi tisa hadi kumi na miwili yaani mwaka mmoja, baada ya upanzi. Dalili za kuwa tayari, mananasi hubadili rangi kutoka kijani hadi ya manjano.

Ekari moja ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 50.

Mauzo yanategemea wateja; wa kijumla huuziwa kwa dazani.

Dazani hugharimu kati ya Sh600 hadi Sh1,000 na kulingana na kilo.

Wateja rejareja huuziwa kwa ukubwa na uzani, ambapo tunda la bei ya chini huwa Sh20.

Baada ya mavuno, mzunguko wa mimea shambani (crop rotation) ni muhimu.

Linalokuzwa mananasi, libadilishwe kwa kupanda mimea kama maharagwe, mpunga, njugu au mboga.

You can share this post!

Kauli ya Ndindi Nyoro kwa Raila Odinga

DP Ruto asisitiza uwaniaji wake wa urais utazingatia amani

adminleo