Habari Mseto

Bob Collymore kuondoka Safaricom 2020

May 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Safaricom imerefusha kandarasi ya Afisa Mkuu Mtendaji Bob Collymore kwa mwaka mmoja.

Kampuni hiyo imesema lengo ni kumfidia mwaka mmoja aliokaa nje alipokuwa mgonjwa. Hii ni kumaanisha kuwa mkurugenzi huyo ataondoka humo mwaka ujao.

“Siendi mahali, nitakuwa hapa kwa mwaka mmoja zaidi, hadi 2020,” alisema Bw Collymore.

Hatua hiyo inachelewesha shughuli ya kutafuta mrithi wa kampuni hiyo aliyopata faida ya Sh63 bilioni mwaka jana.

Mzaliwa huyo wa Amerika Kusini (Guyana) alichukua likizo ya mwaka mmoja 2017 kutibiwa kansa.

Mwezi jana, kulikuwa na ripoti kuwa serikali ilikuwa ikitaka Bw Collymore kurithiwa na Mkenya, na kuifanya kampuni hiyo kuchelewesha kutangaza kiongozi wake mpya.

Safaricom ni kati ya mashirika makubwa zaidi nchini ambayo yanahimili uchumi na ajira nchini. Wakenya hutumia zaidi M-Pesa na kulingana na tetesi, ikiwa huduma hiyo inaweza kuanguka, ni hatari kubwa kwa uchumi.

Safaricom ina watumiaji zaidi ya milioni 30 na hupata zaidi ya Sh200 bilioni kila mwaka.

Pia, kampuni hiyo husaidia maafisa wa polisi kufanya uchunguzi kutokana na mfumo wake mpana.

Vodafone, kampuni mzazi, iliyo na makao yake Uingereza ndio huchagua afisa mkuu mkurugenzi wa Safaricom kutokana na kuwa ilikuwa yenye hisa nyingi zaidi kufikia 2017.

Serikali ya Kenya ina asilimia 35 ya hisa za Safaricom, Vodacom (Afrika Kusini) 35, na Vodafon ina asilimia tano, baada ya kuuzia hisa zake Vodacom.