Mzozo mkubwa baina ya binadamu na ndovu washuhudiwa Subukia
NA PHYLIS MUSASIA
WAKAZI wa kijiji cha Kavilila kaunti ndogo ya Subukia katika Kaunti ya Nakuru wameelezea ghadhabu zao wakisema mamia ya ndovu wamezidi kuvamia mashamba yao na kusabisha hasara.
Wakazi hao wametishia kupanga njama ya kuwaua baadhi ya ndovu hao baada ya maafisa wa usalama wa wanyamapori kukawia kudhibiti hali katika maeneo hayo.
Wakizungumza na Taifa Leo, wakazi hao walisema ndovu hao wameongezeka kutoka 90 hadi zaidi ya 100 na wamekuwa wakivamia mashamba yao na kuharibu mimea tangu Jumanne usiku wiki hii.
“Tumezidi kuumia kutokana na uharibifu ambao ndovu hawa wameendelea kusababisha na tumechoka. Tumejaribu kuwasihi maafisa wa Huduma kwa Wanyamapori (KWS) kujaribu wawezavyo na kuwaelekeza ndovu hawa mahali kunakofaa lakini wamezidi kukawia kufanya hivyo. Kilichobaki kwetu ni labda tupange jinsi ya kuwaangamiza ndovu hawa; labda ni hapo ndipo maafisa watafanya kazi yao,” akatishia mmoja wa wakazi ambaye hatumtaji kwa sababu ya usalama wake.
Kijiji cha Kavilila kiko kwenye mpaka wa kaunti ya Nakuru, Baringo na Laikipia na ndovu hao wanasemekana kuvamia kijiji hicho kutoka kaunti za Baringo na Laikipia ambapo kuna misitu.
Mwakilishi wadi wa eneo hilo Bw David Kiriethe alisema kwamba iasikitisha sana jinsi wakazi wameendelea kuumia kutokana na uvamizi huo na kuwasii maafisa wa wanyama pori kufanya hima na kuhakikisha kuwa hali ya usala inarejea kijijni humo.
“Kijji cha Kavilila kiko mpakani mwa kaunti tatu na ndio maana maafisa wa KWS kutoka katika kaunti hizo wameonyesha hali ya mvutano kuhusu ni timu ipi inapaswa kushughulikia jambo hilo. Hofu imezidi kuongezeka na hata nimepata ripoti kwamba wakazi wametishia kuwamaliza baadhi ya ndovu hao,” akasema Bw Kiriethe.
Hata hivyo afisa wa mawasiliano katika KWS Bw Ngugi Gecaga alipuuzilia mbali madai hayo ya wakazi wa Kavilila huku akisema kuwa tayari maafisa kutoka kaunti ya Baringo wako kule na wamejizatiti kurejesha ndovu hao kule wanakofaa.
“Tulipokea habari hizo mnamo Jumanne na tukawasiliana na maafisa wa Nakuru kwa sababu wao ndio wako karibu na eneo la Subukia. Lakini baadaye tukagundua kuwa wale wa kutoka Baringo ndio wanaweza kushughulikia jambo hilo kwa ukamilifu kwani ndovu hao hutokea sehemu za Baringo na pia Laikipia,” akaeleza Bw Gecaga.
Kuvamiwa na ndovu
Alisema vijiji vingine kama vile Kisanana na Kamasai kule Baringo pamoja na Rongai kaunti ya Nakuru pia vimeripoti visa vya kuvamiwa na ndovu.
“Maafisa wetu wanajaribu sana kuhakikisha kuwa ndovu hao hawaiingii vijijini kwani wanaweza kuwa hatari kwa maisha ya binadamu,” akaongeza.
Masomo katika shule kama vile Kabuswa na Keelbot yametatizika kwani ndovu hao wanasemekana kutumia njia zinazoelekea kwenye shule hizo kufika vijijini.
Wazazi pamoja na walimu walisema wanahofia usalama wa wanafunzi kwani hata wakati wa mchana ndovu hao huonekana wakiwa wamelala kwenye misitu karibu na shule hizo.
“Tumelazimika kutafuta makazi sehemu za juu za Subukia. Na tukiwa huku wakati wa mchana tunaweza kuwaona ndovu hao vizuri jinsi walivyolala msituni,” akasema mkazi mwingine, Bi Grace Chepkoech.
Shughuli za biashara na ukulima ambazo ndizo nguzo za wakazi wengi katika eneo la Kavilila zimekwama kutokana na kutatizika kwa usalama.
Mnamo Jumanne usiku zaidi ya familia 50 zilitoroka makwao baada ya ndovu 90 kuvamia kijiji chao.
Hata hivyo wakazi walisema kufikia Alhamisi idadi hiyo ilikuwa imeongezeka baada ya ndovu zaidi kuvamia mashamba yao usiku uliofuata.
Tayari wamekadiria hasara ya Sh2 milioni.