Maafisa wa EACC wafanya msako katika afisi za Gavana Waititu mjini Thika
Na LAWRENCE ONGARO
MAAFISA wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Alhamisi walivamia afisi kuu za kaunti ndogo ya Thika kwa minajili ya kuchunguza maswala ya ufisadi.
Maafisa hao walifika eneo hilo kwa kishindo huku wakiwa na magari sita tofauti wakiwa wameandamana na maafisa wa usalama zaidi ya 10.
Wafanyakazi waliopatikana afisini waliachwa na mshangao kwa sababu maafisa hao waliingia karibu kila afisi huku wakipekua stakabadhi tofauti wakiuliza maswali hapa na pale.
Wakili mkuu wa Kaunti ya Kiambu Bw Michael Osundwa, alisema maafisa hao wa kupambana na ufisadi walibeba sefu moja ndefu ya futi tano ambayo ilishukiwa kuwa na stakabadhi muhimu.
“Afisa anayehusika na kufungua sefu hiyo hakupatikana mara moja kwani yeye ndiye anahifadhi nambari ya siri inayofungua sefu hiyo,” alisema Bw Osundwa.
Alisema maafisa hao walifanya msako mkali huku wakitaka kuelezwa kila jambo linalohusiana na maswala ya kifedha.
Baada ya msako huo maafisa hao waliwabeba kwa gari lao makarani watatu wa kike ambao hufanya kazi katika kaunti hiyo.
“Makarani hao watatu watakwenda polisi kuandikisha taarifa fulani kuhusiana na uchunguzi huo,” alisema Bw Osundwa.
Maafisa hao walikuwa na shughuli nyingi za kupekua na kukagua mafaili kadha waliyopitia ambapo hata hawakuweza kuzungumza na waandishi wa habari.
Ilidaiwa kuwa baada ya kutekeleza upekuzi huo maafisa hao walibeba vipatakilishi 10 na mafaili kadhaa ili waweze kuchunguza na kuchambua ndani zaidi.
Wafanyakazi wengi walionekana nje ya jengo lao wakinong’onezana kwa sauti ya chini huku wakionyesha hofu katika nyuso zao.
Hakuna mfanyakazi yeyote aliyetamani kuzungumza na mwandishi wa habari kwani waliogopa kuonekana na wakubwa wao.
Mnamo Alhamisi alfajiri, maafisa wa kitengo cha kupambana na ufisadi EACC walivamia makazi ya Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu huku wafanyakazi wengi wakiachwa wakiwaza ni jambo lipi lingine litafanyika kwa gavana wao.
Baada ya kukamilisha shughuli hiyo maafisa hao waliingia kwa magari yao kwa haraka na kuyaondoa kwa mwendo wa kasi bila kuzungumza na yeyote.
Hakuna mwandishi yeyote aliyeweza kuwahoji maafisa hao walionekana walikuwa na lengo moja la kuchukua stakabadhi muhimu.