MAWAIDHA YA KIISLAMU: Funga ni mwalimu wa roho na mlezi wa subira kwa waumini
Leo hii inshaa Allah tutaendelea na mada kuhusu funga ya Swaumu Ramadhan.
Swaumu ni miongoni mwa masomo makuu ya kiamalia ambayo hulenga kumuandaa mfungaji mkweli kuwa mcha Mungu.
Hulenga kumuandaa kukabiliana na magumu ya maisha ya kila siku. Kwa mantiki hii funga huyalea matashi (matakwa), mfungaji akaweza kusema na nafsi yake wakati inapotaka kutenda la haramu au lililo nje ya uweza wake.
Swaumu ni mwalimu anayetoa mafunzo ya kiroho, mafunzo ambayo hupandikiza moyo wa subira katika nafsi ya mfungaji, ili yote haya yapatikane na athari yake ionekane ni lazima mja aitakase ibada yake hiyo, yaani afunge kwa ajili tu ya Allah.
Swaumu kwa maana hii ni mazoezi ya kimwili na kiroho ambayo humtayarisha mwanadamu kukabiliana na matukio ya ghafla yenye kuhuzunisha na kutia simanzi kwa kuwa matukio kama hayo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na hapana budi yatamtokea kama si leo, basi kesho, kwa namna moja au nyingine.
Ikawa hapana budi, mwanadamu huyu aandaliwe na kupatiwa mazoezi ya jinsi ya kukabiliana na kupambana na matukio hayo pindipo yanapojitokeza tena bila ya taarifa.
Yakimtokea asipapatike bali akae chini na kutafakari njia bora ya kukabiliana nayo na kuyatatua. Lolote linaweza kutokea maishani, mtu anaweza kufilisika akawa masikini baada ya kuwa tajiri asiyejua kukosa.
Inawezekana kabisa mtu akawa mgonjwa taabani kitandani baada ya kuwa mzima mwenye siha njema inayomuwezesha kwenda huku na kule na kufanya mambo yake yote mwenyewe.
Si muhali mtu kuwa dhahiri mnyonge baada ya kuwa alikuwa mtu mtukufu mwenye kuheshimika na jamii yake, leo akawa hajulikani tena wala kutajwa.
Inatokea mtu akawa na mke mzuri waliyependana na kuishi maisha mazuri na dhuria (watoto) yao lakini Allah akawachukua wote na kumuacha peke yake bila ya kuwa na wa kumliwaza. Yote hayo na mengine mfano wa haya kuna imkani ya kumtokea mtu katika maisha.
Na ni ukweli usiopingika kwamba matukio haya yana taathira kubwa kwa nafsi.
Taathira ambayo huweza kumfikisha mtu kutoona raha na starehe ya uhai (maisha) huu na hivyo kufikia uamuzi wa kujitoa uhai (kujiua) ili kumuepusha mwanadamu huyu kufika mahala hapo pabaya ni lazima apate mazoezi ya kiamalia ya mwili na roho (swaumu) kila mwaka mara moja kwa uchache. Ili nafsi yake iweze kuzoea kukosa inavyovipenda na kustahamili.
Mtu kusubiri (kustahimili) kuacha kile ambacho ni halali yake ni jambo zito sana, katika nafsi ya mwanadamu kuliko kusubiri kuacha kile kilicho haramu.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa ikiwa mtu ameweza kuitawala nafsi yake na kuacha lililo halali yake, hakuna sababu ya kushindwa kuidhibiti nafsi yake na kuacha lililo la haramu.
Kuacha lililo la halali kunahitaji nguvu na subira nyingi kuliko kuacha lililoharamishwa. Mtu ambaye huitazama neema aliyonayo kwa jicho la amana aliyopewa na Mola wake na anaweza kuichukua wakati wowote.
Mtazamo huu humsahilishia kusubiri kuondoka kwa neema hiyo na kuridhia na kusalimu amri kwa lile alilolikadiria Mola wake.
Ni dhahiri iliyo bayana kwamba kila mwanadamu anahitaji subira katika maisha haya. Mwanafunzi anahitajia sana subira katika kazi yake ngumu ya kulima, ndipo aweze kuvuna matunda ya jasho lake.
Subira yavuta heri
Hata Rais (kiongozi) wa nchi pia anahitajia subira ya kutosha katika kufanikisha kuiongoza nchi.
Kwa ujumla kila mmoja wetu hana budi kuwa na subira katika maisha hata kuishi na watu majumbani, makazini na hata mitaani pia kunahitaji subira.
Kwa hiyo itakudhihirikia kwamba subira ni kitu azizi na muhimu sana katika kurahisisha na kuchanganyika kimaisha.
Ni kutokana na umuhimu na ugumu wa suala zima la subira ndio ikawa ujira wake ni mkubwa usiojulikana ila na Allah pekee, yeye ndiye ajuaye amewaandalia nini wenye kusubiri, tusome:
“… Na bila shaka wafanyao subira (wakajizuilia na maasia na wakaendelea kufanya ya twaa) watapewa ujira wao pasipo hisabu” (39: 10).
Subira hii ni mojawapo ya mafunzo na malezi yanayotolewa na chuo hiki kikuu cha nne cha Uislamu (swaumu).
Chuo hiki kinamuandaa mwanachuo (muumini) kuwa na subira katika kukabiliana na magumu ya maisha ikiwa ni pamoja na kuzoea hali ya kupata na kukosa.
Mwanachuo huyu akihitimu mafunzo yake ya mwezi mmoja chuoni kila mwaka hutunukiwa shahada ya juu ya subira.
Subira ambayo itakuwa ni silaha kubwa katika maisha yake ya miezi kumi na moja ifuatayo baada ya mafunzo.