Makala

Kilio cha mabwanyenye: Nani atarithi mali?

May 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

KUNA taharuki kubwa miongoni mwa mabwanyenye kuhusu urithi wa mali yao baada ya aidha kuzidiwa na uzee au kuaga dunia.

Ni mali nyingi ambayo inaachwa na waliowekeza kwa kujituma na kujinyima raha na anasa na kuishia kuwa na mali si haba lakini hatimaye baada ya kulemewa na uratibu, wanakosa wa kuendeleza mbele mchakato wa uzalishaji mali.

“Ndio kuna shida hiyo na ambayo inakumba wengi wetu ambao wako na mali. Unapata kuwa kuna wenzetu ambao wametangulia mbele ya haki na tunashuhudia wale ambao walitegemewa kusimamia mali hiyo wakilumbana katika kila jukwaa, waking’ang’ania mali hiyo kiasi cha kuzua misururu ya aibu na hatimaye kusambaratisha uwekezaji wote,” anasema Joseph Kaguthi ambaye ni mwekezaji na pia aliyekuwa katika safu ya utawala kwa muda mrefu.

Bw Kaguthi anasema kuwa hakuna ushahidi kuwa mali nyingi iliyo thabiti kwa sasa mikononi mwa wawekezaji wa kibinafsi itasalia thabiti baada ya miaka ya urithi kuingia.

“Kuna shida kubwa ndio. Hawa watoto wetu wako na mzaha sana na jinsi ya kusimamia mali. Unaaga dunia leo, na hata uwe umeacha wosia wa kugawa mali hiyo, unawapata mahakamani wakizozana wagawane upya,” anasema.

Bi Lizzie Wanyoike ambaye ni mwekezaji katika sekta ya elimu na mikahawa anasema kuwa dawa ya kukwepa huu mzozo wa mali ni kuwasajili watoto hao ndani ya biashara hizo.

“Hali hiyo inawapa ule uwezo wa kutambua ugumu wa kuunda biashara hizi. Kwa mfano, mimi nimewapa watoto wangu watatu majukumu ndani ya biashara zangu na wanaelewa kuhusu yote ya faida na hasara kiasi kwamba nikiondoka, watakuwa na uwezo wa kuendelea mbele na biashara hizi,” anasema Bi Wanyoike.

Anasema kuwa kuwapa watoto hao nafasi ya kujifahamisha na biashara za kifamilia huzua ule uhusiano wa moja kwa moja na mikakati ya kuzijenga, hivyo basi kuwapa yale majivuno ya kuhifadhi jina lake kama mwanzilishi kwa miaka mingi ijayo.

Bi Wanyoike anasema kuwa njia nyingine ya kuwapa watoto ule uthabiti wa kubakia pamoja hata baada ya kuachiwa biashara hizo ni kupitia kuwaunganisha pamoja na kuwapa mawaidha ya jinsi umoja huwa ni nguvu.

Anateta kuwa kuna shida kubwa ambapo wengi wa mabwanyenye wanaachia mali zao wasimamizi ndani ya kampuni  za uratibu.

“Kampuni hizo hugeuka kuwa za kupora mali hiyo na hatimaye kuzidisha migogoro ndani ya warithi ili kufanyike maamuzi ya kuuza bidhaa hizo ili waratibu hao waitwae kwa bei za chini,” anasema.

Ni katika hali hiyo ambapo Rais Uhuru Kenyatta anasema kuwa shida kuu ya watoto wengi wa mabwanyenye ni ule ukosefu wa heshima za kimsingi na ulafi wa baadhi yao ambao hugeuka kuwa sumu ya kusambaratisha utajiri huo.

Akiwa katika mazishi ya bwanyenye  Thayu Kabugi aliyezikwa mwezi Aprili katika Kaunti ya Murang’a, Rais alisema kuwa huwa ni aibu kubwa watoto kuzindua awamu za malumbano ya mali baada ya kuachiwa waratibu utajiri.

Baadhi ya familia tajika ambazo kwa sasa zimekubwa na malumbano ya mali ni pamoja na ya  Njenga Karume, aliyekuwa naibu wa rais Kijana Wamalwa na pia bwanyenye Gerrison Kirima.

Wengine ni watoto wa aliyekuwa waziri wa usalama, John Michuki na pia ile ya Hezbone Shimei Nyong’o ambaye ni babake mzazi wa Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o.

Aliyekuwa mbunge wa Makueni na pia jaji, Jackson Mulwa na pia watoto wa James Mwangi Kirung’o ambaye alikuwa mwanzilishi wa Klabu K1 katika Kaunti ya Nairobi.

Pia, kuna watoto wa bwanyenye kutoka Kaunti ya Garissa, Mahat Kuno Roble ambao wanazozania jumba la Almond Resort.

Rais ambaye anafahamika kuwa mmoja wa wengine walio na lao kiuwekezaji anasema kuwa ni sawa na laana kufuja mali iliyokuwa imetafutwa kwa miaka mingi.

Anasema kuwa cha maana ni kuwa na ile heshima ya kuamua kuwa waliozalisha mali wanafaa kuheshimiwa kupitia kuhakikisha mali yao inaendelezwa ili kufaidi wengi kutoka kizazi hiki hadi kile.

Anasema kuwa kwa sasa ana ombi moja tu kwa wanaorithi mali: “Kuunda uwekezaji wa mabilioni huchukua muda na kujituma kwingi. Lakini kuusambaratisha kutachukua hata wiki moja.”

Anawataka wote waliobahatika kuwa na mali iliyoundwa na wazazi wao waelewe kuwa ilikuwa Baraka, na kujaribu kuusambaratisha hugeuka kuwa laana.