Habari Mseto

Zogo la Kibwana, Muthama kuhusu Kalonzo lafufuka

May 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PIUS MAUNDU na GASTONE VALUSI

MZOZO kati ya Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka umechipuka tena huku gavana huyo akimtaka makamu huyo wa rais wa zamani kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Badala yake Profesa Kibwana alimtaka Bw Musyoka kumuunga mkono au mwenzake wa Machakos Alfred Mutua katika azma yao ya kuingia Ikulu, akidai kuwa kiongozi huyo wa Wiper amekuwa akihujumu maendeleo eneo la Ukambani kupitia washirika wake.

Lakini akimtetea Bw Musyoka, aliyekuwa Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama aliwataka wakazi wa eneo hilo kumpuuza Profesa Kibwana akisema gavana huyo hana sifa za kumwezesha kuwa Rais wa Kenya.

“Profesa Kibwana ni upepo unaopita tu. Hana ushawishi wowote hata miongoni mwa jamii za Ukambani wala tajriba faafu kwa afisi kubwa kama urais. Anapoteza wakati wake badala ya kuunga mkono juhudi za kuleta umoja miongoni wa viongozi wa eneo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022,” Bw Muthama alisema Ijumaa alipowahutubia waombolezaji katika kijiji cha Kathithymaa, eneobunge la Matungulu, Kaunti ya Machakos.

Lakini akiongea Alhamisi alipozindua kisima eneo la Kalawa katika Kaunti ya Makueni Gavana Kibwana alisema licha ya wakazi wa Ukambani kusimama na Bw Musyoka tangu 1993, amekuwa akifeli katika kinyang’anyiro cha urais au muungano anaounga mkono kushindwa.

“Tunataka kumwambia kwamba sasa wakati wake wa kutuunga mkono umetimu. Anafaa kutuunga mkono kwa sababu tumemuunga tangu 1993 lakini hakufanikiwa. Tutatuma wazee, akina mama na vijana kwake wamwambie ajiondoe katika kinyang’anyiro cha urasi 2022 na aniunge au ndugu yangu Alfred Mutua,” Profesa Kibwana alisema.

Kuwaleta pamoja wandani

Matamshi ya Profesa Kibwana yanajiri wakati ambapo Bw Musyoka amekuwa akijaribu kuwaleta pamoja wandani wake waliohamia Jubilee katika hatua ya kujiandaa kuwania urais mnamo 2022, licha ya uasi kutoka kwa viongozi kama Profesa Kibwana na Dkt Mutua.

Bw Kalonzo amekuwa akiwafikia wabunge hao wa zamani kupitia ushirikiano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta ambao umefanya baadhi ya wanasiasa hao kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Mandhari ya siasa yamekuwa tulivu kwa miezi kadhaa tangu Profesa Kibwana alipojiuzulu kama mwenyekiti wa Wiper baada ya kutofautiana na Bw Musyoka.

Kulingana na Bw Muthama, Profesa Kibwana anatumiwa na watu ambao wanataka jamii ya Wakamba kugawanyika kuelekea uchaguzi mkuu ujao na hivyo kuzima ndoto ya mmoja wao kuingia Ikulu.

“Profesa Kibwana atajimaliza kisiasa ikiwa hatamuunga mkono Kalonzo kwa wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu ujao. Kibwana hawezi kuwa Rais. Anataka ijulikane kwamba wakati mmoja alitaka kuwania urais kwa kuibua sarakasi zisizo na maana yoyote,” akasema Bw Muthama.

“Naomba jamii ya Wakamba isikubali kupotoshwa kupitia sarakasi za kisiasa zisizo na maana bali itumie wakati huu kusuka umoja wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022,” akawaambia waombolezaji.

Kando na Profesa Kibwana, Dkt Mutua pia ametangaza kuwa atawania urais na amekuwa akizunguka sehemu mbalimbali katika eneo hili kujinadi.