• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Juhudi za kufufua Mumias hatarini kwa kukosa mtaji

Juhudi za kufufua Mumias hatarini kwa kukosa mtaji

Na VICTOR OTIENO

JUHUDI za kufufua Kampuni ya Sukari ya Mumias zimo hatarini baada ya kufutiliwa mbali kwa mpango wa kuiwezesha kupata mtaji.

Vilevile, hatua ya Gavana Wycliffe Oparanya kuisaidia kwa kubuni kamati maalum ya usimamizi wake imepokelewa kwa hisia mseto.

Mnamo Aprili, kampuni hii ilikuwa imetangaza mpango wa kukodisha baadhi ya mali yake, lakini ikausimamisha kutokana na pingamizi kutoka kwa viongozi wa eneo la Magharibi.

Baadhi ya mali iliyopanga kukodishwa ni Uwanja wa Michezo wa Mumias Complex, mkahawa, baadhi ya mashamba, afisi zake, shule za msingi na upili za Booker, nyumba za wafanyakazi wake na duka la jumla.

Mali nyingine iliyopangiwa kuuzwa ni kituo cha kisasa cha kusafisha maji.

“Tungependa kuufahamisha umma kuwa mpango wa kukodisha baadhi ya mali ya kampuni umesimamishwa hadi itakapotangazwa tena,” kampuni ilisema kwenye tangazo.

Na huku Serikali Kuu ikiendelea kunyamaza kuhusu ufufuzi wa kiwanda hicho, tashwishi zimeanza kuibuka ikiwa mpango huo utafaulu.

Katika kile kinachoonekana kama tofauti kuhusu mpango wa ukodishaji, Bw Oparanya alisema kwamba serikali ya kaunti haitawaruhusu watu wachache kuzuia juhudi za kufufua kiwanda hicho.

“Nimewaambia wakurugenzi wa kampuni hiyo kuhudhuria mkutano wa pamoja na wakulima ili kufafanua sababu ya kuamua kuuza mali ya kampuni kupitia mlango wa nyuma. Hii ni hata kabla ya mpango wa kufufua kiwanda hiki kutekelezwa,” alisema Bw Oparanya mapema Mei 2019.

Ni vigumu

Kutokana na kufutiliwa mbali kwa mpango huo, itakuwa vigumu kwa kiwanda hicho kurejelea shughuli zake.

Serikali Kuu ilitarajiwa kutoa Sh2 bilioni kwa ufufuzi wa kiwanda hicho, kutokana na ombi lake mwaka uliopita. Hata hivyo, ombi hilo bado halijatekelezwa.

Kiwanda hicho kinadaiwa Sh700 milioni na wakulima, huku mashirika mbalimbali yakilidai Sh20 bilioni.

Mwaka 2018, Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) ilisema kuwa inakidai zaidi ya Sh1bilioni ambazo hakijalipa kama kodi tangu mwaka 2012.

Jopokazi maalum ambalo lilibuniwa kuchunguza matatizo yanayoikumba sekta ya sukari nchini linatarajiwa kumkabidhi Rais Kenyatta ripoti yake wiki hii, huku kukiwa na madai kwamba ripoti hiyo ilihitilafiwa.

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Uislamu unaruhusu mume na mke kustarehe...

MWANASIASA NGANGARI: Mzungu wa kwanza kuwa waziri baada ya...

adminleo