• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakenya waruhusiwa kutalii mbuga ya Ziwa Nakuru

Wakenya waruhusiwa kutalii mbuga ya Ziwa Nakuru

NA PHYLLIS MUSASIA

MKURUGENZI mkuu wa shirika la Huduma za Wanyamapori Nchini (KWS) Brigedia Msataafu John Waweru Jumapili ameruhusu wananchi kutalii mbuga ya Ziwa Nakuru bila malipo.

Kama mbinu ya kuanza mpango mzima wa kurejesha hadhi ya mbuga hiyo, Brigedia Waweru alitangaza viingilio vya bure kwa Wakenya wote na kuwataka watembee mbugani na kujionea mandhari yaliomo.

“Natangaza haya nikiwa na moyo wa upendo kwa Wakenya wote ambao wangetaka kuzuru mbuga ya Ziwa Nakuru. Najua huu utakuwa ni mwanzo mpya wa kuanza safari ya siku 100 ya kubadilisha hali ilivyo katika mbuga hii,” akasema Brigedia Waweru wakati wa mkutano uliowaleta pamoja washikadau wa maswala ya utalii pamoja na serikali ya Kaunti ya Nakuru.

Aliwasihi washikadau wote kushirikiana kwa kuhakikisha kwamba mbuga hiyo inanyanyua hadhi yake na kufikia ya miaka ya hapo nyuma.

“Mbuga hii ilisifika sana haswa kwa ukuzaji wa ndege aina ya flamingo na watalii wengi walifika hapa kuja kujionea jinsi mandhari yalivyovutia. Imekuwa ni kipindi cha miaka mingi baada ya mbuga yetu kupoteza maana na kusahaulika kabisa,” akasema Waweru.

Mojawapo ya mabasi yaliyotumika kuwapeleka wananchi mbugani Mei 26, 2019. Picha/ Phylis Musasia

Gavana Lee Kinyanjui alipongeza hatua hiyo ya KWS huku akisema serika ya kaunti itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na mashirika mengine ili kuhakikisha kuwa ndoto ya kurudisha uhai katika mbuga la wanyama la Nakuru inatimia hivi karibuni.

Vile vile, Bw Kinyanjui alitoa mabasi ya Kaunti ya Nakuru ili kusafirisha watu katika mbuga na kuwazungusha kwenye safari zao mle ndani.

“Tayari mabasi yanawakusanya wananchi kutoka mjini na kuwapelekea mbugani. Mamia ya watu washapelekewa na mabasi hayo yatatumika pia kuwazungusha kwenye vituo mbali mbugani na kisha kuwarejesha jioni,” akasema naibu wa gavana Dkt Eric Korir kupitia njia ya simu.

Maelfu ya ndege aina ya flamingo wanasemekana kuhama kutoka Ziwa Nakuru baada ya kukosa chakula kwenye maji.

Mwezi Aprili, mbuga hiyo ilishuhudia vifo vya nyati 145 baada ya kuzuka kwa maradhi ya kimeta. Idadi hiyo ililinganishwa na asilimia 3.54 ya jumla ya nyati 4, 100 ambao wanaishi kwenye mbuga hiyo.

Hata hivyi Bw Waweru alitangaza kuwa maradhi hayo yalikuwa yamekabiliwa kwa kikamilifu huku akisema kwamba maafisa wa usalama wa KWS watazidi kuwalinda wanyama wote kwenye mbuga hiyo na kuripoti hali ambazo zinawea kuonyesha dalili za maradhi yoyote.

 

 

You can share this post!

Ajikata nyeti na kuzihifadhi kwa jokofu

Msimu wa masikitiko kwa Barca baada ya kulimwa fainali ya...

adminleo