• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Msimu wa masikitiko kwa Barca baada ya kulimwa fainali ya Copa del Rey

Msimu wa masikitiko kwa Barca baada ya kulimwa fainali ya Copa del Rey

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 30 wa kipute cha Copa del Rey, Barcelona walikamilisha msimu kwa masikitiko makubwa licha ya kuwa na ‘mchawi’ wa kupachika mabao Lionel Messi baada ya kulimwa na Valencia 2-1 katika fainali ya mwaka 2019 mjini Seville, Jumamosi.

Kichapo hiki kinawasili wiki chache baada ya Liverpool kubandua Barcelona nje ya Klabu Bingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 4-3 kwa kuiaibisha 4-0 uwanjani Anfield nchini Uingereza.

Barca, ambao mwezi Aprili walimejitapa watabeba mataji ya Klabu Bingwa, LaLiga na Copa del Rey, walikuwa wameshinda Copa del Rey miaka minne mfululizo kabla ya kuzamishwa na Valencia.

Mabao ya Kevin Gameiro na Rodrigo Moreno yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza yalitosha kunyima Barca taji lingine.

Mwanasoka bora duniani mwaka 2009, 2010, 2011, 2012 na 2015, Messi alifungia Barca bao la kufutia machozi dakika ya 73.

Barca, ambayo sasa imeambulia taji la LaLiga (Ligi Kuu) pekee msimu huu, iliingia fainali ya Copa del Rey na rekodi nzuri dhidi ya Valencia.

Haikuwa imepoteza katika mechi nane katika mashindano yote. Pia, ni mara ya kwanza tangu mwaka 2008 Barca imepoteza dhidi ya Valencia katika Copa del Rey.

Mwaka 2008 pia ndiyo ulikuwa wa mwisho wa Valencia kushinda Copa del Rey kabla ya kupata taji lake la nane kwa kuongeza masaibu ya Barca hapo Mei 25.

Kutoka mikono mitupu katika Klabu Bingwa na Copa del Rey kunatarajiwa kuongeza presha kwa kocha Ernesto Valverde, ambaye alijiunga na Barca mnamo Mei 29 mwaka 2017 na ni majuzi tu aliongeza kandarasi yake kwa mwaka mmoja.

Matokeo haya pia yanatarajiwa kuchochea Barca kujitosa sokoni kwa nguvu katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho kutafuta kujiimarisha kabla ya msimu ujao.

You can share this post!

Wakenya waruhusiwa kutalii mbuga ya Ziwa Nakuru

Lengo la Kahawa Queens ni kutesa mabinti wapinzani ligini

adminleo