• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Unaaibisha Pwani, Kingi amwambia Jumwa

Unaaibisha Pwani, Kingi amwambia Jumwa

 Na PETER MBURU

GAVANA wa Kilifi Amason Kingi sasa amemwambia mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wazi kuwa anawaaibisha viongozi wa eneo hilo, kutokana na siasa ambazo amekuwa akiendesha zisizokuwa na busara.

Gavana Kingi alimshauri Bi Jumwa kuwa na utulivu na heshima, badala ya kuwa na hasira kila mara akikoroga kila mahali anakoenda, akisema ameishia kupoteza heshima.

“Aisha una uchungu- kila mtu anajua, una ghadhabu- kila mtu anajua na una haki ya kuwa na uchungu na ghadhabu kama mwanasiasa. Lakini tumia mbinu nzuri kupigana na janga hili, kuna mbinu zingine ambazo haziwezi kukusaidia,” Gavana Kingi akamwambia.

Alisema hali ya mbunge huyo kuwa na hasira kupita kiasi imeishia kumpotezea heshima, licha ya kuwa analalamika kwa haki.

“Ukimwona mwenda wazimu amevua nguo anakimbia, usivue zako nawe umkimbize ukiwa tupu. Mkifika kule mbele itasemekana wenda wazimu wawili wamepita,” gavana huyo akamwambia Bi Jumwa.

Aliendelea kumzungumzia Bi Jumwa, akimwambia machungu yake yaweza kumsababishia hasara.

“Una hasira lakini hasira hii hatutaki iwe hasara, kuna njia nzuri za kupigana vita hivi na kupata matunda unayolenga. Maanake pale ulipofika sasa, inaanza kutupata aibu kama viongozi,” Bw Kingi akasema.

Kiongozi huyo aliendelea kusema makundi ya Tangatanga na Kieleweke yanapiga siasa sana, kiasi kwamba yanalemaza shughuli za utendakazi serikalini.

“Ili hizi ajenda nne za Rais zitekelezwe kikamilifu, sharti sote kama viongozi wa kisiasa tuwe nyuma ya Rais. Timu mbili ambazo ndizo adui mkubwa wa ajenda nne za Rais wetu ni ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’. Kila wakati wanatusiana na kunyosheana lawama badala ya kuzungumza kuhusu ajenda 4.”

You can share this post!

Tulikupa kazi AU lakini sasa unaharibu sifa ya nchi, Ruto...

Kenya yaburuta mkia London Sevens

adminleo