• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
Uhuru asukumwa kuzima kampeni za mapema

Uhuru asukumwa kuzima kampeni za mapema

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumapili aliendelea kushinikizwa achukue hatua thabiti dhidi ya viongozi wanaoendeleza kampeni za mapema za uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika 2022.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (Cotu), Bw Francis Atwoli alionya kwamba kampeni hizo ambazo zinahusu sana kumpigia debe Naibu Rais William Ruto, zinaweza kutatiza amani nchini.

Alimtaka Rais Kenyatta aingilie kati kama angependa serikali yake ifanikiwe kutimiza ahadi alizotoa kwa Wakenya.

“Rais hafai kuogopa chochote kutoka kwa naibu rais na wandani wake, kwani anaungwa mkono na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga,” akasema Bw Atwoli.

Wito sawa na huo ulitolewa na viongozi wa kike chini ya vuguvugu la Embrace Women Building Bridges Kenya, ambalo limekuwa likizuru sehemu mbalimbali za nchi kuhubiri amani kwa kuunga mkono “handsheki” ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Jana kikundi hicho kilikuwa katika Kaunti ya Baringo.

“Wakazi wa Baringo wanahitaji maendeleo wala sio siasa. Kwa sasa sharti tumheshimu Rais na tumpe nafasi afanye kazi, tuachane na siasa,” akasema Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Wajir, Bi Fatuma Gedi.

Huku hayo yakijiri, vuguvugu lingine lilizinduliwa katika Kaunti ya Nyeri kumpigia debe Dkt Ruto.

Viongozi wa vuguvugu hilo linalotambulika kama ‘Friend of William Ruto’ walisema watakuwa wakizuru maeneo ya mashinani na vituo vya redio vya lugha za kiasili ili kuhakikisha Naibu Rais anajiongezea ufuasi Mlima Kenya.

Ripoti ya VICTOR RABALLA, PETER MBURU Na JOSEPH WANGUI

You can share this post!

Askofu akamatwa kuhusiana na mauaji ya Matungu

Pesa na simu husambaza maradhi – Utafiti

adminleo