Mdahalo ikiwa Raila atagusa kombe la Dunia watawala mitandao
Na ELVIS ONDIEKI na VALENTINE OBARA
MJADALA umeibuka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kama Kinara wa NASA, Bw Raila Odinga, ataruhusiwa kugusa Kombe la Dunia wakati litakapotua nchini kesho.
Wakati kombe hilo lilipoletwa nchini mwaka wa 2013, Bw Odinga, ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu, alikatazwa kuligusa kwa sababu ni marais wa taifa pekee ambao huruhusiwa kufanya hivyo. Wakati huo, rais alikuwa ni Bw Mwai Kibaki.
Hata hivyo, mwaka huu Bw Odinga alijiapisha kuwa ‘rais wa wananchi’ ilhali Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi kwenye uchaguzi wa urais uliofanywa mwaka uliopita.
“Ni rais mmoja pekee anayeruhusiwa kuligusa. Itakuwa ni Uhuru au Baba Raila?” akasema mtumizi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, aliyejitambua kama Elijah.
Kombe hilo litatua Kenya kwa mara ya tatu kesho, baada ya kuletwa mwaka wa 2010 na 2013 kabla mchuano wa kuushindania kufanywa Urusi kuanzia Juni 14 hadi Julai 15.
Kombe hilo la kilo sita lililotengenezwa kwa dhahabu na lenye urefu wa sentimita 36 litaletwa nchini kwa udhamini wa kampuni ya Coca Cola.