Habari Mseto

Ukosefu wa DPP sasa wakwamiza maamuzi mahakamani

February 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KUTOKUWEPO kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kumeacha afisi hiyo kama yatima na idara ya Mahakama katika njiapanda kwa vile imekuwa vigumu kwa mahakimu kutoa maamuzi yenye mashiko kamili ya kisheria.

Kwa mujibu wa katiba ni DPP tu anayepasa kutoa mwelekeo kuhusu kesi na pia kuamuru kufungiliwa kwa mashtaka dhidi ya mmoja.

Hali ya suitafahamu sasa imekumba afisi ya DPP kwa vile maafisa wanaofanya kazi chini yake wanapasa kupokea ushauri na mwongozo kutoka kwa DPP.
Tangu kujiuzulu kwa aliyekuwa DPP Keriako Tobiko, afisi hiyo imeachwa wazi.

Watalaamu wa masuala ya sheria miongoni mwao mwanasheria mkuu aliyejiuzulu Profesa Githu Muigai wamejadilia suala hili pamoja na wakili Donald Kipkorir.

Bw Kipkorir ambaye ni mwanasheria mwenye tajriba ya juu aliambia Taifa Jumapili kwamba kesi zinazofunguliwa wakati huu afisi ya DPP haina afisa baada ya Bw KeriakoTobiko kujiuzulu hazina mashiko ya kisheria.

 

Ajikuna kichwa

Sasa hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani Nairobi Hellen Onkwani anajikuna kichwa iwapo amwachilie raia wa Zibambwe aliye pia kinara wa Kampuni ya Oilibya Kenya Bw Duncan Zinaya Murashika, anayeshtakiwa kwa kuvunja kituo cha kuuza mafuta na kuiba pesa na bidhaa za kampuni ya Maced za thamani ya Sh1.5milioni.

Ombi la kuondolewa kwa kesi dhidi ya Bw Murashika liliwasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Addah Sega.

Bi Sega aliwasilisha kortini barua iliyoandikwa na kutiwa saini na naibu mkuu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (SADPP) James Mungai Warui na kuomba kesi dhidi ya Bw Murashika anayeshtakiwa pamoja na wakenya itamatishwe chini ya kifungu cha sheria nambari 87 (a) za uhalifu (CPC).

Lakini ombi hili lilipingwa vikali na wakili wa kampuni ya Maced Lewis Kyengo anayeitetea akiwa na Kyalo Mbobu akisema “ afisi ya DPP haina afisa anayehudumu na kwamba maagizo ya Bw Warui ya kutamatishwa kwa kesi dhidi ya watano hao itamatishwe ni kutumia idara ya mahakama vibaya.”

Korti imeombwa ikatae hatua hiyo ya Bw Warui na kuamuru kesi dhidi ya Bw Murashiki na wenzake iendelee.

Bw Kyengo alisema Bw Warui kisheria hana mamlaka ya kuamuru kesi itatamatishwe kwa vile yeye sio DPP. Maagizo hayo yamepotoka kisheria.
Pia aliambia korti haki za mlalamishi zitakandamizwa ikitiliwa maanani wakuu hao wa Oilibya walivunja kituo chake cha petroli na kutekeleza wizi.