• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
AUNTY POLLY…: Wananishinikiza nitumie mihadarati

AUNTY POLLY…: Wananishinikiza nitumie mihadarati

Na PAULINE ONGAJI

MWANZONI mwa mwaka nilipojiunga na shule ya upili nilibahatika kukutana na marafiki upesi. Nimegundua kuwa wachache kati yao wanatumia mihadarati na wananihimiza kuungana nao. Nifanyeje?

Jason, 15, Nairobi

Mara nyingi huwa vigumu kuunda uhusiano mpya wa kirafiki au kuvunja mahusiano ya zamani. Siwezi kukuambia ikiwa unapaswa kudumisha au kuvunja uhusiano na mtu fulani. Ni wewe pekee ambaye waweza kufanya uamuzi huo. Kwangu ni kuelekeza tu mambo unayopaswa kuzingatia unapofanya uamuzi huo.

Natumai kuwa umewahi kusikia kuhusu jinsi marafiki wabaya wanaweza kushawishi tabia yako, yaani jinsi watu walio maishani mwako wanavyoweza kushawishi tabia na uwezo wako wa kufanya uamuzi.

Kuna maswali kadha ambayo wapaswa kujiuliza kabla ya kufanya uamuzi huo. Kwa mfano, je, uamuzi huu unakudhuru au kukufaidi? Je, uamuzi huu utakusaidia kutimiza malengo yako? Je, unaambatana na maadili yako? Na je, unafanya hivi kwa minajili yako au yao?

Mihadarati ina hatari kubwa mwilini na akilini mwako, na ikiwa hizi ndizo athari, basi hupaswi kuzitumia.

Kabla ya kushawishika jiulize je, kwa kutumia bidhaa hii utanufaika vipi?

Wajua kila mmoja huwa na viwango vyake vya kimaadili na ndiposa unapaswa kujiuliza iwapo matumizi ya bidhaa hii yanaambatana na maadili na imani yako.

Pia kumbuka kwamba unapofanya uamuzi ili kuwafurahisha wenzio, inamaanisha kwamba huzingatii kuafikia malengo yako.

Maishani unapaswa kuwa na msimamo huku ukizingatia manufaa utakayopata kutokana na hatua unazochukua. Kumbuka kwamba una haki ya kusema la, kila unapokumbwa na shinikizo la kufanya chochote usichotaka kufanya.

Hata hivyo, lazima nikutahadhari kamba huenda ikawa vigumu kufanya hivi. Lakini zaidi ya yote unapaswa kukumbuka kwamba marafiki wa kweli wanapaswa kukutakia mema, na ikiwa hautaki kufanya jambo wanapaswa kukubaliana na uamuzi wako.

Endapo hawako tayari kuunga uamuzi wako hasa unapotaka kufanya jambo la kukunufaisha, basi huna budi ila kukaa mbali na wao.

You can share this post!

MAPOZI: Philip Makanda

Mbwa amjeruhi kibarua sehemu za siri

adminleo