Jeshi la Sri Lanka laeneza msako dhidi ya magaidi
Na AFP
WANAJESHI wa Sri Lanka wanazuilia takriban watu 100, ambao wanashukiwa kuhusika na mavamizi msimu wa Pasaka, ambapo watu 258 waliuawa.
Wanajeshi 3,000 walitumwa katika operesheni ya kusaka washukiwa wa kundi la kigaidi ambalo lilitekeleza mavamizi hayo.
Msako huo ambao ulianzishwa Alhamisi unaendeshwa katika jiji kuu pamoja na miji mingine.
Siku tatu za kwanza za msako, maafisa wa usalama walikamata washukiwa 87.
“Idadi ya watu ambao wanazuiliwa inaweza kuwa 100 kufikia sasa,” afisa wa usalama akasema, akiongeza kuwa takriban wote waliokamatwa walipatikana na ama dawa za kulevya au silaha haramu.
Wengine walikamatwa walipopatikana na kanda za video pamoja na vitu vingine vya kueneza propaganda kuhusu kundi la kigaidi la Natioanal Thowheeth Jama’ath (NTJ), na ambalo limelaumiwa milipuko hiyo.
Kundi hilo limedai kuwa lilishiriki katika mavamizi hayo.
Operesheni kali Jumapili
Sehemu mbalimbali za mji wa Sri Jayawardenepura Kotte zilikuwa zikilengwa katika operesheni hiyo ya wanajeshi mnamo Jumapili.
Misako sawia ya kijeshi ilitekelezwa mkoa wa Kaskazini Magharibi wa Colombo, ambapo maandamano ya kupinga uislamu yalisababisha kifo cha mwanamume mwezi huu, na mamia ya maduka, maboma na misikiti ya waislamu kuharibiwa.
Asasi za usalama zimewakamata washukiwa kadhaa kuhusiana na mavamizi ya bomu, ambapo hoteli tatu na makanisa matatu yalilipuliwa, katika kile kilichoonekana kama vita dhidi ya Wakristo, ambao idadi yao ni ndogo nchini humo.
Wakati maafisa wa serikali wakisema kuwa hatari ya wavamizi hao ilikuwa imeondolewa, Rais Maithripala Sirisena aliendeleza hali ya hatari nchini humo kwa mwezi mwingine.
Sirisena alisema hatua hiyo inanuia kuhakikisha kuwa kuna usalama wa umma, kufuatia mavamizi hayo ya msimu wa pasaka.
Wakristo wanajumuisha asilimia 7.6 ya raia wa Sri Lanka na Waislamu asilimia 10, idadi nyingine ikiwa watu wa imani ya Buddha.
Dunia ilishangazwa na mavamizi hayo ya wakati wa pasaka, ambayo yalisababisha taifa hilo kuomboleza, wakati ulimwengu ulikuwa ukikumbuka kufa na kufufuka kwa Yesu.