• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Polisi wanasa bangi yenye thamani ya kiasi cha Sh5 milioni eneo la Kiandutu

Polisi wanasa bangi yenye thamani ya kiasi cha Sh5 milioni eneo la Kiandutu

Na LAWRENCE ONGARO

POLISI wa Thika wamenasa bangi kiasi cha magunia kumi yenye thamani kubwa katika nyumba moja katika kijiji cha Kiandutu.

Afisa mkuu wa Polisi Thika Magharibi Bi Beatrice Kiraguri alisema Jumatatu wakazi wa kijiji hicho waliarifu polisi kuhusu bangi hiyo.

Alisema gari fulani lilionekana limeegeshwa kando ya nyumba moja huku bangi hiyo ikiingizwa mle ndani majira ya alfajiri mnamo Jumatatu.

“Maafisa wa Polisi walichukua hatua ya haraka kufika mahali hapo na washukiwa walipowaona Polisi walitoroka na kuacha bangi hiyo nyuma,” alisema Bi Kiraguri.

Afisa mkuu wa Polisi Thika Magharibi Bi Beatrice Kiraguri ahutubia waandishi wa habari baada ya kunasa bangi Kiandutu, Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema kulingana na waliokadiria uzito wa bangi hiyo, thamani yake ilikuwa ni Sh5 milioni.

“Tunawashukuru sana wanakijiji wa Kiandutu kwa kuzingatia mpango wa Community Policing, wamefanya kazi na maafisa wa polisi jambo lililofanikisha bangi hiyo kunaswa,” alisema Bi Kiraguri.

Alisema maafisa hao walipata misokoto kadha ya bangi na pia kunasa karatasi aina ya Rizlar.

Mshukiwa awindwa

Alisema tayari wanamfahamu mshukiwa huyo na karibuni watamnasa na kumwasilisha mahakamani kujibu mashtaka.

“Tunashirikiana na wakazi wa kijiji hicho ili kumnasa mshukiwa huyo ambaye amekuwa akiuza bangi kwa wingi eneo la Thika na vitongoji vyake. Tayari maafisa wetu wako mbioni kumtafuta mshukiwa huyo,” alisema Bi Kiraguri.

Miezi mitatu iliyopita polisi mjini Ruiru walinasa bangi ya thamani ya Sh3 milioni katika jumba la mshukiwa mmoja.

Siku chache zilizopita kamanda mkuu wa polisi Kaunti ya Kiambu Bw Ali Nuno aliamuru wahalifu warejeshe silaha walizoficha katika kijiji hicho cha Kiandutu.

Alitoa makataa ya saa 24 la sivyo wahusika wangeona cha mtema kuni.

You can share this post!

Shujaa sasa yahitaji muujiza kusalia katika Raga ya Dunia

Neymar asema atatua Real ikimlipa Sh165m kwa juma

adminleo