• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Hakimu ahofia washukiwa wa mauaji watauawa na polisi

Hakimu ahofia washukiwa wa mauaji watauawa na polisi

NA BRIAN OCHARO

WASHUKIWA watatu ambao wanahusishwa na wizi wa kimabavu na mauaji ya wahudumu wa M-pesa katika kaunti ya Mombasa, wamenyimwa dhamana kwa hofu kuwa watauawa na polisi wakiachiliwa.

Hakimu Mkuu Edna Nyaloti alisema mahakama ina wasiwasi kuwa watatu hao huenda wakapigwa risasi na kuuwa wakiruhusiwa kufuatilia kesi wakiwa nje kwa dhamana.

“Sheria za dhamana zinasema usalama wa mshukiwa lazima izingatiwe kabla ya kuachiliwa kwa dhamana. Nimeridhika kuwa usalama wa watuhumiwa haujahakikishiwa ikiwa watapewa dhamana. Watuhumiwa wanaweza kupigwa risasi na polisi,” alisema.

Hakimu huyo alitegemea karatasi ya afisa wa uchunguzi Fatuma Rajab, ambaye aliiambia mahakama kuwa Brighton Naiya, Mohammed Hassan na mwingine wanahusika kwenye mtandao mkubwa wa kundi la uhalifu ambalo linashukiwa kuwa lilimuua Koplo Jared Oroko.

Bw Oroko aliuawa katika mji wa Taveta, Kaunti ya Taita Taveta wakati alikuwa akifuatilia washirika wa washukiwa katika maficho yao.

Bi Nyaloti alibainisha kuwa, kwa mujibu wa ufunuo wa Bi Rajab kwamba washtakiwa hao pia walimuua Bw Johness Obino, mhudumu wa M-pesa, na haikuwa salama warudi katika jamii.

“Visa vya mauaji na kutoweka kwa vijana ni jambo lilio wazi kwa umma na mahakama hii inafahamu ukweli huo. Amnesty International imechapisha ripoti kadhaa juu ya mauaji hayo, wengi wa waathiriwa ni vijana. Washtakiwa pia wana hatari ya kulengwa na umma,” alisema.

Watatu hao ambao wanadaiwa kuwa sehemu ya kundi la vijana ambao walinaswa kwenye picha za CCTV katika tukio la wizi huko Mikindani, wanashtumiwa kuibia watu sita Sh277, 875 na kuua mhudumu wa M-pesa.

Bw Brighton na Bw Hassan wameshtakiwa kwa makosa saba ya wizi wa kimabavu.

Washukiwa wameshtakiwa kwa kuibia Bw Obino fedha na kumuua katika makazi yake huko Jomvu Aldina.

You can share this post!

Wiper yaanza mbinu za kumwadhibu Kibwana

GWIJI WA WIKI: Jane Kamunya

adminleo