Makala

GWIJI WA WIKI: Jane Kamunya

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na CHRIS ADUNGO

MUNGU alipokuumba, alikupa kipaji ambacho aliwanyima watu wengine wote.

Jihisi kuwa mwenye thamani na kataa kujilinganisha na mtu mwingine.

Ukitanguliza mawazo ya kushindwa katika chochote unachokitenda au unachotarajia kufanya, haitakuwa rahisi kufaulu. Ipo nguvu kubwa ajabu katika kuamini! Jiamini, jikubali na yakatae maisha ya kujihukumu.

Songa mbele kishujaa na ujitabirie mambo makuu katika siku zote za halafu.

Usisahau yote mema ambayo Mungu amekutendea katika uzima na uhai wako. Wengine wanapohesabu idadi ya matatizo yao, wewe endelea kuhesabu baraka zako bila ya kukata tamaa.

Anza kutawaliwa na kiu ya kumpendeza Mungu katika chochote chema unachojishughulisha nacho.

Zaidi ya kumjua, kumtumikia na hatimaye kuishi naye, hii ndiyo sababu nyingine ya Mungu kutuumba.

Huu ni ushauri wa Bi Jane Kamunya – Mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini, kocha maarufu wa tenisi na Naibu Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Gituru, Kaunti ya Murang’a.

Maisha ya awali

Bi Jane Kamunya alizaliwa zaidi ya miongo minne iliyopita katika kijiji cha Karunaini, Kaunti ya Nyeri.

Ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya Bw Joseph Kamunya na Bi Rahab Nyakiunga ambao walihamia baadaye katika Kaunti ya Laikipia.

Kamunya alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Karunaini kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Kimathi, Nyeri mwishoni mwa miaka ya 80.

Wakati huo, Kimathi ilikuwa shule ya mseto na ya kutwa.

Alisomea Kiswahili, Dini na Kwata (PE) katika Chuo cha Walimu cha Kagumo, Nyeri.

Alifunza kwa miaka kadhaa kabla ya msukumo wa kujiendeleza kitaaluma kumchochea kujiunga na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) kusomea shahada ya ualimu katika Kiswahili na Dini.

Alihitimu mwishoni mwa 2008.

Alijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi.

Anatarajia kuhitimu kufikia mwisho wa mwaka huu.

Kamunya anatambua ukubwa wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza vilivyo, kumshauri ipasavyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Anakiri kwamba ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa na kuhamasishwa pakubwa na Bi Gacha aliyekuwa mwalimu wake katika shule ya upili.

Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichapukia Kiswahili alaa kulihali.

Aliyemchochea mno kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Dkt Timothy Arege – mwandishi maarufu wa Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Bi Kamunya amejaliwa mtoto msichana, Rahab Jiks ambaye ni mtaalamu wa masuala ya teknolojia.

Mchango kitaaluma

Baada ya kuhitimu na kufuzu kuwa mwalimu, Bi Kamunya alitumwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kufundisha Kiswahili katika Shule ya Wavulana ya Ituru katika Kaunti Ndogo ya Gatundu Kusini.

Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

“Wanafunzi walianza kuchangamkia sana suala la kushiriki mashindano ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama. Jambo hili lilibadilisha pakubwa sura ya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili shuleni Ituru Boys, nao walimu wakapata hamasa zaidi.”

Wanafunzi wake walimpenda na kuvutiwa sana na upekee wa mbinu zake za ufundishaji.

Kila mwaka, wanafunzi wa Ituru Boys walifaulu vyema zaidi katika mitihani ya KCSE Kiswahili kuliko masomo yote mengine.

Alijulikana zaidi kwa ukakamavu wake wa kukizungumza Kiswahili kwa ufasaha mkubwa popote pale. Si gwarideni, si michezoni, si kanisani, si mikutanoni.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili na baadaye akawa Mkuu wa Idara ya Michezo ili kusimamia drama, tamasha za muziki na uendeshaji wa klabu mbalimbali shuleni Ituru Boys.

Akiwa Mlezi wa Chama cha Kiswahili, alitambua na kukuza vipaji vya wanafunzi anuwai; hasa katika utunzi wa kazi za kubuni.

Kupitia drama na tamasha za kitaifa za muziki, Kamunya alikuwa mstari wa mbele kuwaelekeza wanafunzi wake kutunga mashairi ya kila sampuli na kushiriki michezo ya kuigiza iliyofichua utajiri wa vipawa vyao katika ulingo wa sanaa.

Kwa miaka si haba, wanafunzi wake walitamba sana michezoni huku wakifikia kiwango cha kitaifa kila waliposhiriki tamasha za muziki na drama.

Hapana shaka kwamba Bi Kamunya alichangia sana kubadilisha mtazamo wa wanafunzi wake kuhusu Kiswahili na wakaanza kukichangamkia vilivyo huku wakiandaa na kushiriki warsha na makongamano mengi iwezekanavyo kwa azma ya kuinua viwango vya umilisi wa lugha.

Kwa kushirikiana na walimu wengine wa Kiswahili katika shule mbalimbali za uliokuwa Mkoa wa Kati, walianzisha Chama cha Sanaa ya Kiswahili kwa nia ya kuwanoa wanafunzi kila walipokutana kudhihirisha umahiri wao katika utunzi wa kazi bunilizi, kukariri au kughani mashairi pamoja na kujibu maswali ya kila aina katika masomo ya Lugha na Fasihi ya Kiswahili.

Mapenzi yake ya dhati kwa Kiswahili ni jambo lililomfanya Bi Kamunya kupagazwa jina ‘Binti wa Kiswahili’.

Hivi ndivyo alivyofahamika miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake. Mwishowe, wengi wakawa wanamtambua tu kwa jina ‘Binti’.

Mnamo 2012, alipandishwa cheo na kuwa Naibu Mwalimu Mkuu kisha kupata uhamisho hadi Shule ya

Upili ya mseto ya Gituru katika Kaunti Ndogo ya Kandara, Murang’a.

Anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea pakubwa mtazamo wake kwa masomo anayofundishwa na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Lugha shuleni Gituru, ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mara matokeo ya mitihani ya kitaifa ya KCSE yanapotolewa.

Bi Kamunya anajivunia tajriba pevu katika utahini wa somo la Kiswahili. Uzoefu wake mpana umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kuwahamasisha wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Zaidi ya kuhudhuria makongamano katika jitihada za kuchangia makuzi ya Kiswahili, amewahi pia kualikwa kufundisha, kushauri na kuwaelekeza walimu katika shule mbalimbali za upili ndani na nje ya Kaunti ya Murang’a.

Mnamo 2015, aliweka rekodi ya matokeo bora zaidi baada ya wanafunzi wake kuzoa alama wastani ya 10.3 (B+) katika KCSE Kiswahili. Mwaka mmoja baadaye, alitawazwa Mwalimu Bora (TOYA) katika Kaunti Ndogo ya Kandara na Kaunti nzima ya Murang’a. Aliambulia nafasi ya pili katika eneo pana la Mlima Kenya.

Mbali na kuwa mwamuzi wa kiwango cha kaunti kwenye tamasha za kitaifa za muziki na drama, Bi Kamunya pia ni mwanakamati wa kamati inayoshughulikia elimu katika Kaunti Ndogo ya Kandara. Huhusika sana katika michakato ya kuandaa warsha, midahalo na makongamano yanayoazimia kuboresha viwango vya elimu humu nchini.

Kwa pamoja na walimu wenzake wa Kiswahili Bw Maingi, Bw Muturi, Bi Grace na Bw Nyaga, wameanzisha Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Gituru (CHAKIGI).

Upekee wa chama hiki katika makuzi ya lugha hii ashirafu unatambuliwa sana na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Gituru, Bw Mutero Ndii-Wa ambaye ni mpenzi kindakindaki wa Kiswahili licha ya kwamba yeye ni mwalimu wa somo la Kiingereza.

Uandishi

Bi Kamunya anaamini kwamba safari yake ya uandishi ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Nyingi za insha na mashairi aliyoyatunga yalimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa mwenzake. Isitoshe, ufundi mkubwa katika tungo alilzozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kila sampuli ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanika mno katika ulingo wa Kiswahili.

Anapoendelea kuandika miswada mbalimbali ya hadithi fupi, pia anapania kuchapisha diwani na kitabu kuhusu Uandishi wa Insha.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai azimio la kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili, Kamunya anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Bi Kamunya ambaye ni kocha shupavu wa mchezo wa tenisi, pia ni mfugaji maarufu wa ng’ombe katika Kaunti ya Laikipia.