• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Washukiwa wa mauaji ya Sharon wataka Jaji Lesiit aondolewe kwa kesi

Washukiwa wa mauaji ya Sharon wataka Jaji Lesiit aondolewe kwa kesi

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wawili wanaoshtakiwa pamoja na Gavana Okoth Obado kwa mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno wanamtaka Jaji Jessie Lesiit ajiondoe katika kesi hiyo.

Aliyekuwa msaidizi wa gavana huyo, Bw Michael Oyamo na aliyekuwa afisa mkuu katika gatuzi ya Migori Bw Caspal Obiero walimsihi Jaji Lesiit ang’atuke katika kesi hiyo wakidai atakuwa na upendeleo akiisikiza.

“Tunahofia hatutatendewa haki iwapo utasikiza hii kutokana na matamshi yako hapo awali,” washtakiwa hao walimweleza Jaji Lesiit kupitia kwa mawakili wao June Ashioya na Nelville Amolo.

Mawakili hao walimweleza Jaji Lesiit kwamba alijadilia ushahidi ambao haujawasilishwa kortini alipomwachilia Bw Obado kwa dhamana mwaka uliopita.

Bi Ashioya alimweleza Jaji Lesiit kuwa alisema washtakiwa hao wawili wamelengwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.

“Ulisema katika uamuzi wa dhamana ya Bw Obado kwamba washtakiwa hawa wawili Mabw Obiero na Bw Oyamo walihusika na mauaji ya Sharon na mtoto wake,” alisema Bi Ashioya.

Wakili huyo alimweleza Jaji Lesiit kwamba uamuzi huo uliathiri kesi hiyo ikitiliwa maanani mashahidi waliowataja Mabw Obiero na Bw Oyamo hawajafika mahakamani kuhojiwa kuhusu maungamo hayo.

“Hii mahakama ilikosea kuwahusisha washtakiwa na mauaji ya kinyama ya Sharon na mtoto wake kabla ya kesi kuanza,” alisema Bw Amolo.

Mawakili hao walimsihi Jaji Lesiit ang’atuke kusikiza kesi hiyo kwa vile mawazo yake yamepotoshwa na taarifa za mashahidi.

Bw Amolo alimweleza Jaji Lesiit kuwa hakuzingatia ushahidi wa washtakiwa hao wawili wakikana kata kata kuhusika na mauaji ya Sharon na mwanawe.

Lakini viongozi wa mashtaka Mabw Jacob Ondari, Alexander Muteti na Catherine Mwaniki walipinga ombi hilo la washukiwa hao wawili wakisema “ni njama za kuchelewesha kusikizwa kwa kesi hiyo.”

Watatu hao wamekanusha kumuua Sharon na mtoto wake ambaye alikuwa hajazaliwa.

Obado, Obiero na Oyamo wamekusha walimuua Sharon na mtoto wake mnamo Septemba 21, 2018.

Maiti ya Sharon na mtoto zilikutwa katika msitu wa Kodera ulioko kaunti ya Homabay ukiwa na majeraha.

Jaji Lesiit atatoa uamuzi ikiwa atajiuzulu Julai 19, 2019.

You can share this post!

Si haki Tangatanga kuamriwa wakomeshe kampeni za 2022...

Faini ya Sh1,500 kwa kuramba asali hadharani Uhuru Park

adminleo