• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
NGILA: Tutumie Microsoft kujifua na kuvumisha teknolojia kimataifa

NGILA: Tutumie Microsoft kujifua na kuvumisha teknolojia kimataifa

NA FAUSTINE NGILA

UJIO wa kampuni nguli ya teknolojia kutoka Amerika ya Microsoft katika sekta ya teknolojia nchini umedhihirisha uwezo wa taifa hili katika matumizi ya teknolojia kusuluhisha changamoto za kiuchumi.

Ushirikiano wake na vyuo vikuu nchini ambapo inawekeza Sh10 bilioni, utanoa vipawa vya vijana wetu ambao tayari wamevalia njuga ubunifu wa kidijitali licha ya vizingiti kadha.

Mojawapo ya mipango ya Microsoft ni kuunda mtaala maalum ambao utawaandaa wanachuo kwa soko ibuka la teknolojia hasa katika masuala ya sayansi ya kiotomatiki, roboti, mfumo wa 5G, Blockchain na huduma za intaneti.

Majuzi, nilieleza jinsi teknolojia hizi tayari zimeanza kufanya mageuzi ya kipekee kwa viwanda kadhaa kwa kupunguza muda wa huduma, kuongeza ubora wa bidhaa na kupunguza gharama.

Uwekezaji wa kampuni hii ni zawadi ya aina yake kwa taifa letu, ikizingatiwa kuna mataifa 52 Afrika, lakini Microsoft kwa kutambua bidii zetu katika kuboresha maisha, ikatutunuku fursa hii nadra kutusaidia kukabili vizingiti ambavyo vimekuwa vikitutia breki.

Katika ushirikiano huu, wahadhiri wa sayansi ya kompyuta na teknolojia wanafaa kujitolea vilivyo kuwapa wanafunzi ujuzi ambao wameukosa kwenye mtaala.

Ni dhahiri kuwa tutanufaika pakubwa kutokana na hatua ya kampuni hii, hasa kupitia kueneza ujuzi kwa mataifa mengine Afrika ambayo tayari yanatuona kama magwiji wa teknolojia.

Hatua hii pia itaisukuma serikali kupitia Wizara ya Teknohama kuboresha mazingira ya uwekezaji wa teknolojia, na kuchukulia masuala ya ubunifu kwa uzito zaidi. Kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu, tunafaa kuona idadi ya wahadhiri wa teknolojia ikiongezwa.

Tukifuata nia hii, tutashuhudia kampuni changa zikichipuka kutoka kila eneo la nchi kwani Microsoft inashirikiana na vyuo vyote nchini, na kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira nchini.

Kulingana na uelewaji wangu, ili mpango kama huu uzae matunda, serikali inafaa kujenga vituo vya sayansi na utafiti katika kila chuo, ili kuunda mtandao thabiti wa teknolojia wa kukuza talanta.

Mataifa yote yaliyopiga hatua kiteknolojia yana vituo hivi, ambapo ubunifu umezaa teknolojia endelevu zinazotumika duniani kote kama Facebook, Twitter, Amazon, Android, Alibaba na Tesla.

Tusiwe tu watumizi wa teknolojia zilizoundwa na wazungu wakati wote, tutumie fursa hii kubuni teknolojia zetu ambazo zitaweza kutamba kimataifa. Nina imani tele kwamba tuna uwezo wa kuunda mifumo ya kidijitali ambayo itakubaliwa kote duniani.

[email protected]

[email protected]

You can share this post!

Kalameni atiwa adabu kukwepa kulipia danguro

WANDERI: Utamaduni wa Mwafrika tiba ya matatizo ya ndoa

adminleo