• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
ONYANGO: Tangatanga wasionewe, sote hutoa hela chafu kanisani

ONYANGO: Tangatanga wasionewe, sote hutoa hela chafu kanisani

Na LEONARD ONYANGO

KWA takribani miezi miwili sasa kumekuwa na mjadala mkali kuhusu ikiwa makanisa yanafaa kukubali au kukataa michango kutoka kwa wanasiasa wanaodhaniwa kuwa wafisadi.

Wanasiasa wa kundi linalofahamika kama ‘Kieleweke’ wametufanya kuamini kwamba michango inayoyotolewa na Naibu wa Rais William Ruto pamoja na wanasiasa wanaomuunga mkono ni chafu na haifai kukubaliwa makanisani.

Kundi la kieleweke pia limetufanya kuamini kwamba michango inayotolewa na wanasiasa wanaopinga Dkt Ruto kuwania urais 2022 ni safi na inakubalika mbele za Mungu.

Porojo hizo za kupotosha zinazoenezwa na kundi la Kieleweke zimesababisha baadhi ya viongozi wa makanisa mbalimbali wakiongozwa na mkuu wa Kanisa la Kianglikana humu nchini Jackson Ole Sapit, kupiga marufuku michango kutoka kwa wanasiasa wanaoshukiwa kuwa wezi wa fedha za umma.

Ukichunguza ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, utabaini kwamba hakuna mbunge, gavana, seneta au diwani aliye safi.

Ripoti ambazo zimekuwa zikitolewa na Bw Ouko kuanzia Januari, mwaka huu, zinaonyesha kuwa ufujaji wa fedha za umma umekolea katika Hazina za Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) zinazosimamiwa na wabunge na serikali za kaunti.

Kwa mfano, ripoti iliyotolewa na Bw Ouko mnamo Februari, ilionyesha karibu maeneobunge yote 290 yalifuja sehemu kubwa ya Sh5 bilioni zilizotolewa na serikali ya kitaifa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Kulingana na Bw Ouko, maeneobunge hayo hayakuwa na stakabadhi za kuonyesha jinsi fedha hizo zilivyotumika. Uwezekano mkubwa ni kuwa fedha hizo ziliishia mifukoni mwa wabunge husika pamoja na wasimamizi wa NG-CDF.

Ukizingatia Biblia ambayo Wakristo wanaitumia kama mwongozo utabaini kwamba hakuna ‘wizi mdogo’ na ‘wizi mkubwa’ – wizi wote ni sawa mbele za Mungu. Katika Amri Kumi, Mungu alisema ‘Usiibe’ kwa maana kwamba mwizi wa Sh50 na mwizi wa Sh20 milioni wote wamekosa mbele za Mungu.

Ikiwa mhudumu wa bodaboda atamwibia mteja wake chenji ya Sh50 na akazipeleka kanisani kama sadaka na mwanasiasa aibe Sh15 milioni pia azipeleke kanisani; wote wamempeleka Mungu hela za wizi.

Hiyo inamaanisha kwamba wengi tumekuwa tukipeleka fedha zilizo na dosari kanisani.

Makanisa yamekuwa na mtindo yakiwekeza katika ujenzi wa mahoteli ya kifahari badala ya kujenga vituo vya kulea watoto mayatima na waathiriwa wa dawa za kulevya. Wamegeuza kanisa kuwa biashara.

[email protected]

You can share this post!

WANDERI: Utamaduni wa Mwafrika tiba ya matatizo ya ndoa

NGUGI: Wamchao Mungu wana majukumu zaidi ya kuhubiri

adminleo