IEBC yasubiriwa kuidhinisha sahihi za Thirdway Alliance kutoa nafasi kwa kura ya maamuzi
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA watashiriki kura ya maamuzi ikiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itathibitisha sahihi 1.4 milioni zilizowasilishwa kwake na Chama cha Thirdway Alliance Kenya kinachoongozwa na mwanasheria Ekuru Aukot.
Shughuli ya kuthibitishwa kwa sahihi itaendelea kwa muda wa majuma mawili ambapo chama hicho kimeelezea matumaini kuwa tume hiyo itahakikisha uhalali wa sahihi hizo zote.
“Ni matumaini yetu kwamba katika IEBC shughuli ya ukaguzi wa sahihi hizo haitaingiliwa kisiasa. Hii kura ya maamuzi ni muhimu kwa sababu inalenga kuwapunguzia Wakenya mzigo unaowakabili sasa wa kiuchumi,” Bw Aukot aliwaambia wanahabari Jumatano katika kikao na wanahabari katika makao makuu ya chama chake, Nairobi.
Kwenye kampeni yake kwa jina Punguza Mzigo, chama cha Thirdway Alliance Kenya kinapendekeza kupunguzwa kwa idadi ya wabunge katika mabunge yote mawili kutoka 416 hadi 194, na kufutiliwa mbali kwa viti vya manaibu Gavana pamoja na nafasi za madiwani maalum.
Chama hicho pia kinapendekeza kuwa Katiba ifanyiwe mabadiliko ili Rais awe akihudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba.
Mswada
Ikiwa IEBC itaridhika kuwa chama hicho kimetimiza hitaji la kikatiba la kukusanya angalau sahihi milioni moja kutoka kwa Wakenya waliojisajili kuwa wapiga kura, itawasilisha mswada huo kwa mabunge 47 ya kaunti ili upigiwe kura.
Ikiwa mswada huo utapitishwa na angalau mabunge 24 utawasilishwa katika bunge la kitaifa na Seneti
Wabunge wa ODM juzi waliitaka serikali kutenga pesa katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya kufadhili kura ya maamuzi.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi wabunge juzi walisema kuwa watazunguka kote nchini kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa shughuli hiyo.
Viongozi hao wanapendekeza kubadilishwa kwa sura kuhusu utawala ili kubuniwa wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili.
Pendekezo hilo pia linaungwa mkono na Baraza la Kitaifa la Makanisa (NCCK).
Hata hivyo, Naibu Rais William Ruto na wabunge wanaounga mkono azma yake ya kuwania urais wanapinga pendekezo hilo wakisema cheo cha Waziri Mkuu hakitawanufaisha wananchi wa kawaida bali wanasiasa wachache.
Huku mjadala huo ukiendelea kushika kasi, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi anasema hakuna maandalizi bora yamefanyika kwani sheria husika haijabuniwa.
“Bunge kupitia Kamati kuhusu Sheria na Masual ya Kikatiba kwanza inapaswa kubuni sheria ambayo itaongozwa kura ya maamuzi kabla ya zoezi hilo kufanyika. Mjadala unaoendelea sasa ni siasa tu.” Bw Muturu akaambia Taifa Leo.