Michezo

Danny Rose haamini Spurs wamo fainalini

May 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

BEKI wa kushoto, Danny Rose wa Tottenham Hotspur amesema aliona kama ndoto pale klabu hiyo ilitinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Nyota huyo wa kimataifa amesema klabu hiyo imepiga hatua kubwa tangu ujio wa kocha Mauricio Pochettino, miaka mitano iliyopita.

Rose amesema aliona kama miujiza wakati klabu hiyo ilipoziangusha njiani timu kubwa kama Manchester City na Ajax Amsterdam kwenye mechi ngumu za robo fainali na nusu-fainali ambapo Lucas Maura alifunga mabao matatu.

“Tangu nijiunge na klabu hii, mawazoni sijawahi kufikiria habari za kucheza fainali ya Klabu Bingwa,” alisema Rose.

“Akili yangu ilikuwa tu kwa mataji ya Carabao Cup na FA Cup pamoja na ligi kuu (EPL). Tulitinga fainali ya Carabao na mara mbili kucheza katika nusu-fainali ya FA Cup, lakini hatukufaulu. Kwa sasa, tumepata fursa kubwa ya kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa, kitu ambacho sikufikiria kingenipata hapa; kwa kweli nimeamini chochote chaweza kufanyika katika soka.”

Tangu ajiunge na klabu hii, Pochettino amekuwa akiwakumbusha wachezaji wake kwamba wana uwezo wa kukabiliana na klabu kubwa ambazo zimekuwa zikitawala soka barani, na sasa Rose anaona ujumbe huo umefaulu.

“Sasa nimeelewa alichokuwa akisema. Kujiamini katika kila jambo ni muhimu hasa kwa wachezaji. Mwanzo sikuwa namuamini. Lakini sasa naelewa, hiyo imedhihirisha uwezo wake katika majukumu yake ya ukufunzi,” aliongeza.

Kocha awaamini vijana

Spurs hawakununua mchezaji mwingine tangu Moura awasili Januari 2018 akitokea Paris Saint-Germain (PSG), hali ambayo imekuwa ikiwafanya baadhi ya wachezaji akiwemo Rose kulalamika, lakini Pochettino aliendelea kuwaamini wachezaji alio nao.

“Nimekuwa nikishangaa ni kwa nini kocha hafikirii kuleta wachezaji wapya, lakini sasa nimemuelewa baada ya kutufikisha fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kuangusha timu kubwa njiani,” alisema staa huyo.

“Kocha wetu anajiamini, anatuamini, na Sote tuko nyuma yake kwa lolote lile. Kwa sasa mawazo yetu yanalenga ubingwa wa Klabu Bingwa, na michuano ya ubingwa huu, msimu ujao. Pongezi zimuendee kocha kwa kazi nzuri. Sote tunstahili pongezi.”

Spurs wanakutana na Liverpool ugani Wanda Metropolitano jijini Madrid, Uhispania hapo Jumamosi kwenye fainali hiyo na Rose anasisitiza motisha ya wachezaji wote iko juu tangu msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) umalizike.

“Kile ambacho kocha anaendelea kutuambia ni kutulia na kuichukulia mechi hii kama nyingine yoyote ile, bila kuwadharau wapinzani wetu,” alisema.

“Kocha anataka tuingie uwanjani na tutende tulivyowatendea Ajax na Manchester City katika mechi za awali za kufuzu; ana matumaini makubwa nasi tumejiandaa vya kutosha na kila mtu anaisubiri fainali kwa hamu na ghamu dhidi ya Liverpool,” aliongeza.

Spurs hawajawahi kushinda taji la Ulaya tangu wanyakue ubingwa wa UEFA Cup mnamo 1984 na Rose anaamini wakati umetimia kwa kikosi cha sasa kuweka historia mpya.

“Hakuna aliyedhania tungefika hapa kabla ya michuano hii kuanza. Hata wengi hawakufikiria tungetinga robo-fainali na hata nusu-fainali,” alisema nyota huyo wa umri wa miaka 28.