• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Miguna Miguna asimulia yaliyomkuta

Miguna Miguna asimulia yaliyomkuta

Na SAMMY WAWERU

WAKILI Miguna Miguna amesema akipata pasipoti yake hatasita kurejea nchini mara moja ili kuendelea kutetea haki za wananchi.

Bw Miguna amesema kinachomzuia kuwa nchini ni kutokuwa na hati hiyo ya usafiri na kwamba hakuna anachohofia kuwepo nchini.

Alifurushwa nchini mara mbili mwaka uliopita, 2018, katika kile kilitajwa kama kutekeleza kosa la uhaini kumuapisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kama Rais wa Wananchi, na ambaye kwa sasa anashirikiana kwa karibu na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Wakati wa matukio hayo, kizaazaa kilishuhudiwa katika uwanja wa kimataifa wa JKIA.

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen kipindi cha JKL Jumatano usiku, Miguna alisema ni heri afe “kifo cha hadhi wakati akitetea haki za wanyonge sawa na mashujaa waliopigania uhuru”.

“Ni heri nife kihadhi nikitetea wanyonge ili katika wasifu yangu watu wajue nilikuwa mtu wa aina gani,” alisema, katika kipindi hicho kinachoendeshwa na mtangazaji Jeff Koinange. Mahojiano hayo yalipeperushwa moja kwa moja kutoka Washington D.C., Amerika.

Katika simulizi ya masaibu aliyopitia wakati wa kukamatwa kwa wahusika wakuu kumuapisha Bw Raila Januari 30, mwanaharakati huyu alisema mawakili wake walinyimwa fursa kumuona.

“Waikwa Wanyoike ambaye ni wakili tajika kutoka Canada alikatazwa kuniona. Badala yake waliruhusu Winnie Odinga (mwanawe Raila), ambaye si wakili. Nilimlalamikia kwa nini kinara wa muungano wa Nasa hakuonekana. Raila Odinga alipokuja, nilichofanya ni kumsalimu pekee, tukaelekea katika lango la kutoka lakini lilifungwa,” akasema, akionekana kutilia shaka ziara ya kiongozi wa ODM JKIA.

Bw Miguna Miguna alilalamikia mazingira duni aliyohifadhiwa, ikiwa ni pamoja na kusafirishwa kutoka kituo kimoja cha polisi hadi kingine Kiambu.

“Waliniibia kila kitu nilichokuwa nacho, kibeti changu kilikuwa na dola 1,500 za Marekani (sawa na Sh150,000 thamani ya Kenya). Wakati nikiwa JKIA, nilitiwa katika chumba ambacho nilipoteza fahamu nikajipata Dubai nisijue mahala pa kuanzia,” alieleza.

Alisema kurejea nchini bila pasipoti ya Kenya, hataruhusiwa kuendesha shughuli zozote hasa kushiriki siasa, licha ya kuwa raia wa Kenya kwa njia ya kuzaliwa. Unapozuru taifa lolote, unapaswa kuwa na pasipoti ya kukuruhusu kuingia humo.

Mwanaharakati huyu alijitangaza jenerali wa vuguvugu la NRM ambalo liliharamishwa na Wizara ya Usalama wa Ndani.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 uliohusisha mrengo wa Jubilee ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Nasa chini ya kinara wake Raila Odinga, mvutano ulizuka kuhusu matokeo ya urais ya Agosti 8.

Nasa ilipinga matokeo hayo, ikidai yaliborongwa na Jubilee ili isalie madarakani.

Ni kufuatia mvutano huo Nasa ilielekea katika mahakama ya juu zaidi, kilele chake kikawa matokeo kuharamishwa na tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka IEBC kuagizwa kuandaa marudio ya uchaguzi kiti cha urais, ingawa muungano huo haukushiriki.

Ghasia zilizuka haswa katika ngome za Nasa, watu kadhaa wakiripotiwa kuuawa na hata kujeruhiwa vibaya wakati maafisa wa usalama wakishika doria.

Machi 9, 2018, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta walifanya salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki, ambazo zilipunguza joto la kisiasa. Bw Raila kwa sasa anashirikiana sako kwa bako na serikali kufanya maendeleo.

You can share this post!

Ruto akera ODM ‘kumpa Raila kazi ya Uwaziri Mkuu...

Gor kusaka nyota wa kigeni kuijaza nafasi ya Tuyisenge

adminleo