HabariSiasa

Nikikumbuka uchochole ulivyonitesa utotoni, mimi hutoa mamilioni kanisani – Ruto

May 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto ametumia mkutano wa maombi ya kitaifa Alhamisi kuelezea sababu yake ya kutoa michango katika makanisa kila wikendi.

Dkt Ruto alisema kuwa Mungu amemwinua kutoka katika umaskini hivyo anarudisha shukrani kwa aliyofanyiwa.

“Acha nikiri hapa kwamba Mzee Jomo Kenyatta alipofariki dunia mnamo 1978, nakumbuka vyema nilikuwa nachunga ng’ombe na niliposikia kwamba rais amefariki nilipeleka mifugo nyumbani nikifikiri ulikuwa mwisho wa dunia,” akasimuliwa Dkt Ruto.

Akaendelea; “Mnamo 1980 nilifanya mtihani wa kitaifa wa kukamilisha elimu ya msingi na sikuwa na viatu wakati huo kwa sababu hivyo ndivyo tulikuwa. Baba yangu alininulia viatu mara ya kwanza mnamo 1981 kutoka kwa jamaa aliyekuwa anaitwa Bw Onyango kwa Sh60.”

Dkt Ruto alisema ni kwa neema ya Mungu ambaye amemfanya kuwa miongoni mwa watu waliofanikiwa nchini.

“Unaona leo mtu ambaye hakuwa na viatu leo anaishi ameketi katika meza ya waheshimiwa pamoja na mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya (Rais Uhuru Kenyatta),” akasema Dkt Ruto.

Michango ambayo imekuwa ikitolewa na Dkt Ruto makanisani imezua mjadala mkali huku wapinzani wake wakitaja fedha hizo kuwa za wizi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji Jumatano aliwataka wakuu wa kidini kukoma kupokea hela kutoka wanasiasa kama njia mojawapo ya kukomesha ufisadi.

Baadhi ya viongozi wa kidini, wakiongozwa na mkuu wa kanisa la Anglikana humu nchini Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit, tayari wamepiga marufuku michango kutoka kwa wanasiasa.

“Ukiona baadhi yetu tunaenda kanisani na kuomba, kuinua mikono, kulia na hata kutoa michango ni kwa sababu tunakumbuka mahali Mungu ametutoa. Nawaomba kuelewa hili,” akasema.