Imamu atandika muumini katika msikiti wakiomba
TOM MATOKE na GERALD BWISA
FUJO zilizuka katika msikiti mmoja mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi, baada ya Imamu kumtwanga magumi muumini mnamo Jumatano jioni.
Waumini wengine walitoroka katika msikiti huo wa Kapsabet Jamia kabla polisi kuwasili na kutuliza hali.
Habari zilisema Imamu huyo alirushiana maneno makali na mwumini huyo kabla yao kukabana koo na kulishana makonde wakati wa sala ya jioni.
Mashahidi walisema mwumini huyo alimkaripia Imamu kuhusiana na barua ambayo mhubiri huyo alikuwa ameandikia polisi, akidai mwumini alikuwa mwenye itikadi kali za Kiislamu na kwamba alihusiana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Mkuu wa Polisi Nandi ya Kati, Bw Stephen Wambua alithibitisha kuwa mhubiri na mwumini waliandikisha taarifa.
“Tutafanya uchunguzi kuhusu kisa hicho na ukikamilika tutawafikisha kortini,” Bw Wambua aliambia Taifa Leo.
Baadhi ya waumini walimshutumu Imamu huyo kwa kutumia maneno machafu dhidi ya Waislamu wenzake msikitini, kinyume na mafunzo ya dini.
“Tunafaa kuwa wanyenyekevu na watulivu mwezi huu wa mfungo wa Ramadhani, na fujo zozote zinafaa kushutumiwa kabisa,” akasema Shekhe Dawood ambaye ni mmoja wa maimamu katika msikiti huo.
Kwingineko, pasta mmoja mjini Kitale aliokolewa na polisi kutokana na hasira za wananchi waliotaka kumpa adabu kwa madai ya unajisi.
Pasta huyo wa Impact Healing Ministries alikabiliwa na umati baada ya mlinzi mmoja kupiga kamsa kwamba alikuwa amemvizia binti mdogo ofisini mwake.
Kulingana na mlinzi huyo Peter Wafula, msichana huyo alitaka kuonyeshwa ofisi ya pasta na walipokaa zaidi ya saa moja humo ndani mlinzi huyo aliingia shaka.
Pasta na msichana walipelekwa katika kituo cha polisi cha Kitale walikolala seli kabla msichana kupelekwa keshoye katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kitale kufanyiwa uchunguzi wa kubaini iwapo alidhulumiwa kimapenzi.
“Ripoti ya uchunguzi wa matibabu ilisema hakukuwa na ishara za msichana kushiriki ngono na pasta huyo, lakini bado tunaendelea kuchunguza kisa hicho,” alisema Kamanda wa Polisi Kaunti ya Trans Nzoia, Bw Ayub Ali.