Habari Mseto

Wavulana na wasichana wa Iterio wembe mkali maigizoni

March 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ANTHONY NJAGI

SHULE za Iterio Girls na Iterio Boys zilisisimua katika mashindano ya Kaunti ya Kisii ya Uigizaji kwa shule za sekondari yaliyoandaliwa katika Chuo cha Walimu cha Nyabururu.

Wavulana wa Iterio Boys waliibuka simba katika michezo ya kuigiza wakifuatwa na Nyakoiba nao Mobamba wakamaliza katika nafasi ya tatu.

Verah Orare wa Shule ya Upili ya Masongo akariri shairi ‘Red rage” akiongozwa na Dkt George Aroba katika mashindano ya Maigizo Kisii Machi 1, 2018. Picha/ Anthony Njagi.

Iterio Boys walisisimua hadhira kwa mchezo wao uliofahamika kama “Pandemonium” ambao uliwasilisha ujumbe kuhusu ubinafsi unavyotatiza juhudi za kuleta umoja wa kitaifa.

Mwandishi wa mchezo huo, Franklin Nyambane alielezea matumaini yake kuwa mchezo huo utafika hadi mashindano ya kitaifa yatakayoandaliwa Nairobi.

Shule ya Upili ya Kerongorori yacheza densi ya kitamaduni katika mashindano ya maigizo kaunti ya Kisii Machi 1, 2018. Picha/ Anthony Njagi.

Nao wanadada wa Iterio waliibuka washindi katika kitengo cha Densi ya Kisasa na kufuatwa na Masongo Secondary huku Nyatieko wakimaliza katika nafasi ya tatu.

Katika ukariri wa shairi la mtu mmoja, Nyamonaria walichukua nafasi ya kwanza wakifuatwa na Cardinal Otunga na Masongo mtawalia.

Kuhusu shairi la makundi, Kisii School waliwika wakifuatwa na Mobamba Secondary huku Kioge Girls wakimaliza wa tatu.

Celestine Nyakania na Naomi Osoro wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Nduru wasimulia hadithi katika mashindano ya maigizo yaliyofanyika kaunti ya Kisii Machi 1, 2018. Picha/ Anthony njagi.

Katika Densi ya Kitamaduni, Sengera Girls walipepea mbele ya Babaracho na Ogorera.

Shule ya Mobamba Secondary nayo ilinyakua ushindi katika hadithi ikifuatwa na Gesabakwa katika nafasi ya pili huku Kisii School ikimaliza katika nafasi ya tatu.

Bogeka Secondary nao waliibuka washindi katika sarakasi wakifuatwa na Mobamba katika nafasi ya pili mbele ya Magena Girls.