Timu ya voliboli ya wanaume yapanga kurekebisha makosa kutafuta tiketi ya African Games

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kukosa makala yaliyopita kwenye michuano ya voliboli ya Bara Afrika ya Wanaume ya African Games, Kenya itakuwa makini kutumia uwanja wake wa nyumbani kupata tiketi ya kurejea katika mashindano ya mwaka 2019 yatakayofanyika Agosti 19-31 nchini Morocco.

Kenya itaalika Tanzania, Uganda, Misri na Rwanda jijini Nairobi kutoka Juni 3-7 katika mchujo wa Ukanda wa Tano wa kuwania tiketi ya kuelekea jijini Rabat.

Vijana wa kocha Moses Epoloto, ambaye anasaidiwa na Paul Muthinja, wamejawa na motisha, ingawa wamekiri kibarua kigumu kinawasubiri hasa dhidi ya Misri na Rwanda zilizowakilisha eneo Ukanda wa Tano katika African Games jijini Brazzaville nchini Congo mwaka 2015.

Wapinzani wa Kenya wanatarajiwa kuwasili jijini Nairobi hapo Juni 2.

Wanawake wa Kenya walifuzu zaidi ya juma moja lililopita jijini Kampala nchini Uganda. Malkia Strikers, jinsi timu hiyo inafahamika kwa jina la utani, ilichapa Rwanda, Ethiopia na Uganda kwa seti 3-0 kila mmoja na kujikatia tiketi kutetea taji nchini Morocco.

Ratiba:

Juni 3

Uganda na Misri (2p.m.)

Tanzania na Kenya (4p.m.)

Juni 4

Rwanda na Tanzania (2p.m.)

Kenya na Uganda (4p.m.)

Juni 5

Uganda na Rwanda (2p.m.)

Misri na Kenya (4p.m.)

Juni 6

Tanzania na Uganda (2p.m.)

Rwanda na Misri (4p.m.)

Juni 7

Misri na Tanzania (2p.m.)

Kenya na Rwanda (4p.m.)

Habari zinazohusiana na hii