Habari

Ramaphosa atangaza baraza jipya la mawaziri, asilimia 50 ni wanawake

May 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

RAIS Cyril Ramaphosa ameandikisha historia kwa kuteua asilimia 50 ya wanawake katika baraza lake jipya la mawaziri.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa letu, nusu ya mawaziri wote ni wanawake,” kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66 akasema katika hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja katika kituo cha runinga cha taifa hilo.

Katika hotuba aliyotoa jijini Johannesburg, Ramaphosa alisema amepunguza idadi ya mawaziri kutoka 36 hadi 28 kwa kuunganisha baadhi ya idara na wizara kwa lengo la kupunguza gharama.

“Hatua hii pia itaimarisha utendakazi wa serikali na uwiano wa kitaifa,” Rais huyo akaongeza.

Bw Ramaphosa alisema raia wote wa Afrika Kusini wanafahamu kwamba taifa hilo linakabiliwa na changomoto za kiuchumi na kupanda kwa gharama ya maisha.

“Kwa hivyo, serikali hii italenga kufufua uchumi na huku ikihakikisha kuwa pesa za umma zinatumiwa kwa uangalifu,” akasema.

Rais Ramaphosa aliapishwa Jumamosi na kuwa Rais wa sita nchini humo kuwahi kuchaguliwa kidemokrasia.

Baraza lake jipya la mawaziri linajumuisha watu kadha wenye umri mdogo. Aidha, wengine wameshangazwa na hatua ya Ramaphosa kumteua kiongozi wa upinzani Patricia De Lille kuwa Waziri wa Ujenzi na Miundombinu.

Aliyekuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi Tito Mboweni amedumisha wadhifa wake wa Waziri wa Fedha huku Pravin Gordan akiteuliwa Waziri wa Utumishi wa Umma.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga