UMBEA: Ndoa nyingi zavunjika sababu ya maigizo wakati wa uchumba
Na SIZARINA HAMISI
PILIKAPILIKA za mahaba huwafanya baadhi ya watu waishi maisha yasiyo halisi wakati mwingine.
Hasa kwa wachumba ambao badala ya kuishi maisha yao halisi, wanaishi ili kufurahisha wenzao na wakati mwingine kutenda mambo ambayo sio halisi.
Katika hali hii wapo wanaodiriki kukopa ama kuchukua hatua za ziada ili kuwafurahisha wawapendao.
Changamoto ni kwamba hali hii ikiendelea hadi unapowadia wakati wa ndoa, kunakuwa na athari nyingi ambazo zinaweza kuleta shida katika ndoa husika.
Ndoa nyingi za vijana siku hizi huvunjika mapema sababu ya kuishi maisha ya uigizaji kipindi cha uchumba. Kwamba kijana utajidai kuishi maisha ambayo siyo yako na labda huna jinsi ya kuyamudu.
Kiasi kwamba mchumba ama mpenzi wako anapotembelea nyumbani kwako anakuta jokofu limejaa mchanganyiko mbalimbali wa vinywaji na chakula, huku ukimweleza kwamba jokofu lako haliwezi kuwa tupu hata siku moja.
Wakati unajua bayana kuna siku huwa makazi ya mende na maji ya kunywa, sababu ya kukosa uwezo wa kulijaza hizo bidhaa unazodai hazikosekani wakati wote.
Mnapopanga mkutane, unachukua hatua za ziada kujipiga msasa na kujiweka katika hali ya kuvutia na kunukia ili kumvutia zaidi mwenzako.
Kwamba siku zote unapokutana na mwenzako ni lazima uhakikishe ni nadhifu na kuvutia.
Hakuna siku ambayo mwenzako amekuona ukiwa katika hali yako halisi, wakati mwingine ukitoa harufu ya kikwapa ama pia mdomo ukiwa unanuka kama choo cha jiji.
Kwamba hata ile miito halisi pia unajibana na kwenda kuifyatua faraghani, kiasi kwamba mwenzako anadhani labda huwa huendi msalani wakati mwingine.
Mkilala sasa, ndio vimbwanga vingine, yaani inaitwa kulala kwa ustaarabu.
Kila mmoja analala kwa tahadhari asikorome wala asiache mdomo wazi, tena unapoamka unakimbilia bafuni kupiga mswaki ili kuondoa harufu mfu mdomoni.
Kwamba huyo mwenzako hajawahi kukutana na kombora la harufu mara unapofungua mdomo asubuhi.
Sinema hii inaendelea hadi wakati wa mlo, pale unapotoka na mwenzako na mkaagiza chakula, kila mmoja atajidai kuagiza vyakula vya kistaarabu, utasikia nataka soseji, chipsi mara mkate wa kuoka mara kuku mpinduko.
Utajidai hujui wala kutambua githeri, ngwashe, mukimo, muthokoi au dagaa wa nazi.
Rafiki yangu udanganyifu huu utakufikisha wapi?
Patashika huanza pale mnapofunga ndoa kabla ya kuonyesha uhalisia wenu. Kila siku mpo wote kuthibitisha uhalisia wa maisha yenu ya uchumba. Sasa sijui mtaweza kuendelea na maisha ya maigizo. Na hapo ndipo unaanza kumchosha mwenzako na hatimaye usaliti, hadaa na lawama huanzia hapa.
Ni vyema kuishi maisha halisi tangu mkiwa wachumba ama mnapoanza uhusiano. Kuleni ugali, dagaa, muthokoi na hata githeri bila chuki wala hadaa.
Kuleni ndizi, viazi choma, mahindi choma au hata mahindi ya kuchemshwa. Wakati mwingine shindieni mizambarau, machenza au hata malenge.
Hata unapoamka asubuhi, msalimie ukiwa na uvundo mdomoni, hata kabla hujaenda kuswaki na kuwa na hali shwari mdomoni. Siku nyingine kuwa katika hali halisi ya mavazi, yale unayovaa ukiwa umepumzika nyumbani ama ukiwa unaenda kuona rafiki yako wa karibu bila kujali atasemaje.
Dada, uhalisia ni nguzo kubwa katika uhusiano. Kwani siku zote ukweli utakuweka huru. Kuwa wazi kwa mwenzako na iwapo anakupenda kwa dhati hatajali wala kukuhukumu. Ukiona mwanaume anakutenga sababu ya mavazi ama hali yako fulani, basi ni wazi hana mapenzi ya dhati kwako. Sasa unajua cha kufanya.