Wafisadi katika Wizara ya Ugatuzi hawana pa kujificha – Marwa
Na MOHAMED AHMED na WINNIE ATIENO
KATIBU wa Wizara ya Ugatuzi, Nelson Marwa ameapa kupambana na ufisadi katika wizara hiyo. Bw Marwa alisema kuwa kikosi maalum kimeundwa ili kupambana na ufisadi.
“Mambo ya ufisadi hamtasikia tena. Kile mutaona ni huduma kwa wananchi wote,” akasema Bw Marwa.
Visa vya madai ya ufisadi viliwahi kukumba wizara hiyo wakati wa muhula wa kwanza wa uongozi wa Jubilee.Kesi hizo za ufisadi zilipelekea kujiuzulu kwa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kama waziri.
Bw Marwa alisema kuwa kikosi hicho kitafuatilia kwa makini namna utendaji kazi utakavyoendeshwa chini ya ugatuzi.
Akizungumza katika hoteli ya Travellers wakati wa warsha ya majadiliano kuhusu ugomvi kati ya serikali kuu na zile za kaunti, Bw Marwa alisema magavana watafuatiliwa kuhusiana na namna wanavyotumia rasilimali za wananchi wanazopata ndani ya ugatuzi.
“Kila Mkenya ni muhimu kwetu. Tuko na magavana wanaoelewa namna mambo yanatakiwa kufanywa. Kwa hivyo lazima wapeane huduma bora kwa wananchi,” akasema Bw Marwa.
Alisema kuwa kuna haja ya kuwa na mpangilio ambao utahusisha kila Mkenya na sio mpango wa kufaidisha wachache.
“Ugatuzi ni lazima upeane heshima kwa wananchi. Kuhudumia Wakenya kwa njia sawa ndio lengo la kila wizara hivyo basi mwananchi lazima ahusishwe,” akasema.
Kwingineko, Kamati ya Seneti inayohusika na matumizi ya fedha za umma itaanza kutathmini miradi yote inayotekelezwa na magavana katika kaunti 47.
Pia, inataka kuhakikisha magavana wanatekeleza wajibu wao na hawafuji mali ya umma.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Moses Kajwang alisema mjini Mombasa kwamba shughuli hiyo itaanza Aprili.
Kugatua mikutano
Akiongea kwenye mkutano wa kamati hiyo katika hoteli ya Sarova Whitesands, Bw Kajwang alisema kamati hiyo imeamua kugatua mikutano yao ili Wakenya wawe na imani na ugatuzi.
“Mara kwa mara huwa tunapata ripoti kuhusiana na miradi iliyotekelezwa na magavana bila ya kutathmini ukweli kuhusiana na miradi hiyo ya maendeleo.
Lakini sasa tumebadilisha mtindo kwani tutaenda mashinani kudadisi miradi hiyo kabla ya kupitisha ripoti hizo,” akasema Bw Kajwang ambaye pia ni seneta wa Homabay.
Hata hivyo baraza la magavana limeitaka kamati hiyo ihakikishe magavana hawadhalilishwi kama hapo awali, walipokuwa wakihojiwa na kamati hiyo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Josphat Nanok alisema magavana wataitikia mwito ili kueleza kuhusu miradi na maswala yoyote tata yatakayoibuka.
“Sioni tatizo lolote kwa magavana kuitwa ili kuweka wazi swala lolote ibuka katika serikali za ugatuzi sababu ni wajibu wetu. Lakini kuwe na maelewano ili tushirikiane si kama hapo awali ambapo kulikuwa na utata mkubwa baina ya magavana na kamati,” Bw Nanok ambaye alihudhuria kikao kingine huko Mombasa akajibu.
Bw Nanok ambaye pia ni gavana wa Turkana aliitaka kamati hiyo kuwalenga wahusika badala ya kuwakandamiza magavana.