Makala

DAU LA MAISHA: Bila ujuzi wala uzoefu kajitosa katika ujenzi

June 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

BILA tajiriba, ni wanawake wachache ambao wana ujasiri wa kujitosa katika sekta zinazotawaliwa na wanaume hasa ya ujenzi.

Ni hisia alizokumbana nazo Agnes Onyancha, 44, alipoamua kujitoma katika fani ya ujenzi.

Mambo yalikuwa magumu zaidi hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa na digrii ya masuala ya Mauzo na shahada ya uzamili katika masuala ya Ujasiriamali; taaluma tofauti kabisa na kazi hii.

Bi Agnes Onyancha akiwa katika sehemu mojawapo ya mradi anaosimamia. Picha/ Hisani

Lakini hakuacha hofu yake, vile vile ukosefu wa tajriba vizime ari yake ya kujihusisha na ujenzi, huu ukiwa mwaka wake wa tano sasa tangu ajitose ndani.

Yeye ni mkurugenzi wa kampuni ya Houseman General Contractors, shirika linalohusika na masuala ya ujenzi wa nyumba za makazi na hata za kibiashara.

Tangu 2013 amehusika katika miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwa ni pamoja na nyumba na afisi kadha za haiba ya juu.

“Chini ya ungalizi wangu, kampuni hii imehusika katika ujenzi wa zaidi ya majengo kumi ya haiba ya juu, ambapo kazi yangu hasa inahusisha kupanga miradi, kuifadhili na kuhakikisha kwamba inakamilika,” asema.

Kulingana na Bi Onyancha, siri yake ni uzoefu ambao amekuwa akipata jinsi anavyoendelea kuhudumu na ambao umekuwa ukiimarika kutokana na penzi lake katika kazi hii.

Aidha, anasema kwamba mapato mazuri yamechangia kwake kukwamilia humo na kamwe hana nia ya kurejea kuhudumu katika kazi yake ya zamani.

Kiu yake ilianza mwaka wa 2013 alipoacha kazi yake ya afisi.

“Nilikumbwa na mwasho wa kutaka kukamilishia wateja miradi, na hivyo nikakata kauli. Pia msukumo huu ulitoka kwa mume wangu ambaye tayari alikuwa anaendesha kampuni hii,” aeleza.

Lakini licha ya ufanisi huu, Bi Onyancha anasema kwamba safari hii haijakosa changamoto.

“Kazi hii inachukua muda mwingi kiasi kuwa wakati mwingine unajipata hauna muda wa kujumuika na wenzako,” aeleza.

Aidha anazungumzia dhana inayohusisha kazi hii na wanaume na uchafu vilevile.

Lakini anasema hajaacha tatizo hilo limnyime usingizi katika jitihada zake za kujiundia jina katika sekta hii.

Kinyume na matarajio ya wengi, dhana hii potovu imekuwa kichocheo chake kwani anasema imemfanya kuhisi spesheli na kumpa nguvu na moto wa kufanya vyema zaidi.

Kazini pazuri

Japo kwa baadhi ya watu huenda wanatarajia mwanamke kukumbana na mazingira makali kazini, Bi Onyancha anasema kwamba kwake mambo yamekuwa tofauti.

“Kwanza kabisa nimeajiri watu werevu; wa kike na wa kiume, kumaanisha kwamba wanaheshimiana na wana uhusiano wa kawaida kazini. Lakini pia nilibahatika hasa ikizingatiwa kwamba tayari mume wangu alikuwa akiendesha biashara hii,” asema.

Ni kazi ambayo imemletea heshima kubwa sio tu kutoka kwa wafanyakazi wake, bali pia famila yake kwa jumla.

“Mume na watoto wangu wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi zangu,” aeleza.

Anasisitiza kwamba kujihusisha na kazi hii kamwe hakujapunguza sifa zake za kike.

“Kuna baadhi ya watu huenda wakadhani kwamba katika kazi hii sina muda wa kuonekana mrembo. La! huo sio ukweli. Kama wanawake wengine nina muda wangu wa kujipodoa, kupendeza na kuonyesha sifa zangu za kike. Mara nyingi mimi hupata muda wa kufanya hivi siku za Ijumaa ambapo kazi huwa imepungua kiasi,” asema huku akiongeza kwamba kwa sasa madhumuni yake ni kupata fursa zaidi kupanua biashara yake.