TAHARIRI: Harambee ina fursa nzuri ya kufana Cairo
Na MHARIRI
HATA ingawa maneno kadhaa ya kashfa yamesemwa kuhusiana na uteuzi wa kikosi cha Harambee Stars, pana mambo kadhaa mazuri kuhusu mipango ya timu hiyo yanayohitaji kutambuliwa.
Kwanza, hii inakuwa mara ya kwanza kwa kikosi cha taifa kukita kambi barani Ulaya -penye sifa nyingi za mafanikio ya soka – kwa maandalizi ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) linaloanza mwezi huu wa Juni nchini Misri.
Harambee Stars imeelekea nchini Ufaransa kwa maandalizi ya takribani wiki mbili kabla ya kuenda Misri kwa dimba hilo linalong’oa nanga Juni 21, 2019.
Ikiwa huko, timu hiyo ya taifa chini ya kocha Sebastien Migne, ambaye naye ni raia wa Ufaransa, itajipima nguvu na timu mbili za Afrika; Bukini (Madagascar) jijini Paris kisha kuelekea Uhispania ambapo itapambana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uzuri wa kujiandaa nchini Ufaransa ni kwamba, mbali na hali ya hewa inayokaribiana na Misri, kocha huyo anaweza kutumia uraia wake kuwashawishi wajuzi mbalimbali wa soka nchini humo kuwapa Harambee Stars mashauri ya kitaalamu yanayoweza kuwafaa watakapokuwa wakichuana na miamba wa soka barani Afrika.
Kenya imepangwa pamoja na timu ngumu; nambari moja barani, Senegal na miamba wengine Algeria pamoja na jirani zake Tanzania. Hivyo basi, timu hii ambayo imecheza fainali hizo za bara mara tano, itahitaji kutumia maarifa, ujuzi na maandalizi mazuri kufanya makuu, vinginevyo, hali haitakuwa rahisi kwa timu hizi za Afrika ya Mashariki.
Kocha huyo anahitaji kuungwa mkono anapofanya maamuzi yake muhimu kuhusu kikosi kitakachobeba bendera ya taifa jijini Cairo, Misri.
Japo kwa vipimo vya mashabiki wa kawaida mkufunzi huyo amewaacha nje baadhi ya wanasoka wazuri, huenda kwa vigezo vya kitaalamu alifanya linalofaa kufanywa. Kwa sababu hiyo hafai kuhukumiwa kwa ubaya jinsi inavyoonekana.
Anastahili kutiwa motisha ndiposa apate ari ya kuwatia motisha na ujasiri wanasoka wake kuanzia pale wawapo katika kambi ya mazoezi hadi kwenye fainali zenyewe.
Kwa upande mwingine, serikali kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) pamoja na wahisani wapige jeki kikosi hicho katika suala la pesa ndipo kiweze kujiandaa vyema. Kwa sasa timu hiyo ilitengewa Sh250 milioni pekee; pesa ambazo kwa kweli huenda zisitoshe kwa maandalizi mazuri pamoja na kushiriki fainali zenyewe.