• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
MWANASIASA NGANGARI: Ndiye alikuwa ‘Mfalme wa Ameru’ kwa kipindi kirefu

MWANASIASA NGANGARI: Ndiye alikuwa ‘Mfalme wa Ameru’ kwa kipindi kirefu

Na KYEB

MIAKA ya mwisho ya uhai wake, Jackson Harvester Angaine alijijenga kama “Mfalme wa Meru”, akikumbukwa kama waziri ambaye alipewa wizara ngumu zaidi baada ya uhuru, ambayo ilishughulika na kuwapa mashamba Wakenya waliokuwa maskwota, katika mashamba yaliyokuwa ya Wazungu.

Vilevile, alikuwa mmoja wa waafrika ambao walimiliki mali nyingi na mashamba, hali ambayo ilisababisha kuwa na tofauti kubwa za utajiri baina ya Wakenya, wengine wakimiliki mali na wengine kukosa.

Alizaliwa mnamo 1900 katika kijiji cha Gautuku, kata ya Ntima, Meru. Alijiunga na shule ya kimishenari ya United Methodist, Kaaga kwa masomo ya shule ya msingi mnamo 1913, kisha akaenda Alliance, ambapo alisoma na Odinga.

Alikuwa mwana wa chifu mkuu Angaine M’Itiria na katika shule ya Alliance alipenda mchezo wa ubondia.

Baada ya masomo hayo hakujiunga na chuo kikuu, ila alianza kazi ya uhasibu.

Safari yake ya kisiasa ilianza alipojiunga na chama cha KAU na akawa mwenyekiti wake wilaya ya Meru. Wakati huo, KAU hakikuwa na kiongozi wa kitaifa wa kuunganisha wafuasi, lakini kurejea kwa Kenyatta kutoka Uingereza kulikiwezesha kujipenyeza sawasawa.

Huku Kenyatta akikiongoza na kwa kushirikiana na wanasiasa wachanga, KAU kilijipenyeza katika eneo la Gikuyu, Embu na Meru, kisha kikaanza kupenya kitaifa. Hapo ndipo Angaine alikuwa kiongozi wake wa Ameru, cheo ambacho kilimpaza katika siasa za kitaifa.

Kuibuka kwa vuguvugu la Maumau miaka ya 1950 hadi Uhuru aidha kuligusa siasa za Meru, kwani kwa hali kuwa eneo la Meru lilikuwa jirani na Mlima Kenya, shughuli nyingi za vuguvugu hilo zilifanyikia huko.

Mnamo Oktoba 9, 1952, chifu mkuu aliyekuwa ameteuliwa kusimamia uongozi wa ukoloni eneo la Mlima Kenya Kung’u Waruhiu aliuawa kwa kupigwa risasi na wapiganaji wa Maumau, hatua ambayo iliwafanya wakoloni kuanza kuchukua hatua dhidi ya uongozi wa KAU, wakisema ndio ulichochea.

Takriban wiki mbili baada ya Waruhiu kuzikwa, hali ya dharura ilitangazwa na operesheni ya kuwasaka viongozi wa KAU katika jamii za Gikuyu, Embu na Meru ikaanzishwa. Maelfu ya Wakikuyu, Waembu na Wameru walikamatwa, uchumi wa eneo la kati ukiathirika.

Angaine alikamatwa na akazuiliwa Kajiado, Mackinon Road, Hola na kisiwa cha Manda. Katika jela ya Manda, alipoteza meno kwa kuteswa, na kwa kuonekana kama mhalifu sugu alikuwa nusura auawe kwa kunyimwa chakula.

Msukumo wa kutafuta uhuru, hata hivyo, ulichacha, Gichuru (Martin), (Oginga) Odinga na (Tom) Mboya wakisukuma kupatikana kwa haki kwa wote. Angaine aliachiliwa kutoka jela na akajiunga na viongozi wengine wa KAU, wakati chama cha KANU kilipozinduliwa mnamo Machi, 1960, Kiambu.

Katika uchaguzi wa 1961-kwenye maelewano ya katiba iliyoundwa katika kongamano la Lancaster- chama cha KANU kilibwaga chama pinzani cha KADU kwa kushinda asilimia 67.5 ya kura zote, na Angaine akashinda moja kati ya viti vya Meru.

Mnamo 1962 wakati serikali ya muungano iliundwa baada ya Lancaster, aliteuliwa kuwa katibu wa bunge (waziri msaidizi) katika wizara ya Utalii, Misitu na Wanyama pori, kisha wizara ya Elimu.

Alipoingia serikalini, ustadi wake kiusimamizi ulijitokeza na kufikia wakati uchaguzi mkuu wa 1963 uliandaliwa, Angaine alikuwa mmoja kati ya viongozi wakuu wa Meru waliojulikana, hivyo kwa urahisi akachaguliwa mbunge wa Meru Magharibi.

Matarajio makuu

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Kenyatta, ambapo kulikuwa na matarajio makuu kuwa watu ambao ardhi zao zilitwaliwa na wakoloni zingerejeshwa, lilikuwa jukumu la Angaine kutofautisha kuhusu hali ya kiuchumi na matakwa ya kisiasa kwa kufanya hivyo.

Watu waliokuwa na uwezo wa kiuchumi kiasi walihisi kuwa ikiwa mashamba yaliyokuwa ya wazungu yangeathirika, uchumi ungezorota, lakini wengine, hasa waliopigania uhuru walitaka mashamba hayo. Mashirika kama Benki ya Dunia na wafadhili wengine pia walikuwa wakitaka utaratibu kufuatwa kwa kufanya zoezi hilo.

Angaine, hata hivyo, licha ya changamoto nyingi na Benki ya Dunia kufanya kila juhudi kuingilia zoezi la watu kupewa mashamba aliibuka kama waziri mwenye usemi zaidi wakati wa kugawa mashamba hayo. Aidha, aliibuka kama mmoja wa waliomiliki mashamba makubwa zaidi nchini.

Mnamo 1976, usemi wake ulimfanya mmoja wa mawaziri wa ngazi ya juu walioendesha kampeni iliyoanzisha na viongozi wa Muungano wa Gikuyu, Embu na Meru (Gema), ya kubadilisha katiba.

Miaka miwili baadaye, Kenyatta alikufa na Moi, ambaye Angaine hakutaka aongoze akaapishwa Rais. Angaine na wenzake waliotaka katiba ibadilishwe walitengwa katika serikali na katika uchaguzi mkuu wa 1979 akapoteza kiti chake kwa Nteere Mbogori.

Mambo yalizidi kumharibikia Angaine kwa kuibuka kwa wanasiasa wapya kama Matthew Adams Karauri (Tigania) na Kirugi M’Mukindia (Imenti ya Kati). Aidha, maskwota walivamia shamba lake la ekari 4,000 eneo la Timau na kuanza kuishi.

Mnamo 1983, hata hivyo, alirejea na akambwaga Mbogori. Hapo, aliteuliwa waziri katika afisi ya Rais, ambalo lilionekana kama pigo kisiasa.

Ni wakati huo ambapo alijiita “Mfalme wa Meru”, japo wanasiasa wachanga kutoka Meru walikuwa wakifanya juhudi kumwondoa kama mkuu wa Kanu katika wilaya ya Meru.

Kuingia kwa siasa za vyama vingi aidha kulibadili mkondo wa siasa Meru, kwani kuondoka kwa Mwai Kibaki kutoka KANU (wakati huo akiwa Makamu wa Rais) na kuunda chama cha DP kulifanya KANU kupoteza umaarufu eneo hilo.

Katika uchaguzi wa 1992 Angaine alipoteza ubunge wa Imenti Kaskazini kwa David Mwiraria, na hapo kufifia kwa safari yake kisiasa kukaanza. Baadaye alipoteza uenyekiti wa KANU wilaya ya Meru wadhifa ambao alikuwa ameshikilia tangu uhuru.

Majaribio ya kumkuza mwanawe, Mutuma, ili aongoze pia hayakuzaa matunda, japo alikuwa akiamini kuwa angerejea tena.

Hata hivyo, umri mkubwa na matatizo ya kiafya hayangemruhusu. Alirejea nyumbani kwake Timau, ambapo alifanya kilimo, kisha akatoweka kutoka siasa za kitaifa.

Mnamo Februari 23, 1999, Angaine alifariki, akiacha watu kumkumbuka kwa jukumu lake la kugawa mashamba baada ya uhuru. Kufaulu ama kufeli kwake katika zoezi hilo ndiko kunaamua ikiwa alikuwa mwanasiasa aliyefaulu, japo eneo la Meru, hakuna mwanasiasa mwingine anayeweza kuongoza kisiasa, jinsi Angaine aliongoza.

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke

You can share this post!

DINI: Unavyoyamalizia maisha yako ndio muhimu, haijalishi...

Ole wao walioficha mamilioni

adminleo