Kazi rahisi kwa Prisons na Pipeline baada ya droo ya voliboli
Na GEOFFREY ANENE
DROO ya mashindano ya voliboli ya Klabu Bingwa Afrika ya wanawake imefanywa, huku wawakilishi wa Kenya, Pipeline na Prisons, wakiwekwa katika makundi yanayoonekana rahisi.
Mabingwa mara saba Pipeline wamo Kundi C ambalo pia linajumuisha washindi wa medali ya fedha mwaka 2017 El Shams (Misri), FAP (Cameroon), DGSP (Congo Brazzaville) na Vision (Uganda). Tishio kubwa hapa kwa Pipeline ya kocha Japheth Munala ni Shams na FAP.
Prisons ya kocha David Lung’aho, ambayo inajivunia mataji matano ya Afrika, italimana na INJS (Cameroon), Customs (Nigeria), Douanes (Burkina Faso) na Asec Mimosas (Ivory Coast) katika Kundi D. Katika kundi hili, Prisons na INJS zina uzoefu wa miaka mingi.
Mabingwa mara nane Al Ahly (Misri) wako kundi A pamoja na Nkumba (Uganda), Nyong (Cameroon) na Rwanda Revenue Authority (Rwanda). Mkenya Dorcas Ndasaba ndiye kocha mkuu wa wawakilishi hawa wa Rwanda.
Mabingwa watetezi Carthage (Tunisia) watalimana na Harare (Zimbabwe), Chlef (Algeria), Bafia (Cameroon) na Botswana Defence Force katika Kundi B.
Timu mbili za kwanza kutoka makundi haya manne zitaingia robo-fainali.
Vikosi vya timu za Kenya:
Pipeline – Trizah Atuka (nahodha), Noel Murambi, Leonida Kasaya, Celestine Nafula, Monica Biama, Naomi Too, Rose Jepkosgei, Yvonne Sinaida, Janet Wanja, Agrippina Kundu, Rael Tebla, Esther Wangeci, Lucy Akinyi na Christine Ngugi. Benchi la kiufundi – Japheth Munala (kocha mkuu), Margaret Indakala (kocha msaidizi)
Prisons – Mercy Moim (nahodha), Joy Luseneka, Herma Jepyegon, Loise Jepkosgei, Edith Wisa, Emmaculate Chemtai, Shyrine Jepkemboi, Diana Khisa, Lorine Chebet, Everlyne Makuto, Sharon Chepchumba, Yvonne Wavinya, Elizabeth Wanyama na Judith Tarus. Benchi la kiufundi – David Lung’aho (kocha mkuu), Josp Barasa (kocha msaidizi).