• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Miamba wa soka duniani

Miamba wa soka duniani

NA MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

LIVERPOOL walifuta kumbukumbu za kupoteza fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu jana kwa kuwapepeta Tottenham Hotspur msimu huu kwa mabao 2-0 na kutawazwa wafalme.

Nyota Mohamed Salah aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao katika dakika ya pili baada ya kiungo Moussa Sissoko wa Tottenham kunawa mpira ndani ya kisanduku.

Bao hilo lilikuwa kitulizo kikubwa kwa Salah, fowadi mzawa wa Misri aliyelazimika kuondoka uwanjani mapema wakati wa fainali ya msimu uliopita baada ya kuumizwa na beki Sergio Ramos wa Real Madrid.

Japo fainali hiyo haikushuhudia mihemko na ushindani mkali uliotawala mikondo miwili ya nusu-fainali, Tottenham ndio waliomiliki asilimia kubwa ya mpira katika vipindi vyote viwili.

Baada ya kuwazidia maarifa wapinzani wao katika takriban kila idara, Tottenham walipata nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo zingaliwazalia mabao muhimu iwapo kipa Allison Becker asingalijituma zaidi langoni.

Becker ambaye kwa sasa ni mlinda-lango ghali zaidi duniani, aliyapangua makombora mengi aliyoelekezewa na wavamizi Son Heung-Min, Lucas Moura na Christian Eriksen.

Kusuasua kwa Tottenham kuliwachochea zaidi Liverpool kurejea mchezoni mwishoni mwa kipindi cha pili na hivyo kujipata wakiadhibiwa vikali na Mkenya raia wa Ubelgiji, Divock Origi.

Origi aliyejaza nafasi ya Roberto Firmino katika dakika ya 70, aliwazidi ujanja mabeki wa Tottenham kirahisi kabla ya kumwacha hoi kipa Hugo Lloris ambaye awali, alikuwa pia amefanyizwa kadi nyingi za ziada na mchezaji matata mzaliwa wa Senegal, Sadio Mane aliyeongoza safu ya mbele ya waajiri wake.

Kocha Mauricio Pochettino alilaumiwa pakubwa kwa maamuzi yake ya kumwajibisha nahodha Harry Kane ambaye hakuwa amecheza mchuano wowote tangu Aprili 2019 kutokana na jeraha baya la kifundo cha mguu.

Kane alichezeshwa katika nafasi ya Moura aliyewatambisha Tottenham pakubwa katika mkondo wa pili wa marudiano ya nusu-fainali dhidi ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi.

Liverpool walinyanyua ufalme wa UEFA ambao kwa mujibu wa kocha Jurgen Klopp, masogora wake walinyimwa msimu jana baada ya Salah kujeruhiwa bega mapema katika fainali iliyochezewa jijini Kiev, Ukraine.

Ushindi wa kikosi hicho unamaanisha kwamba Liverpool kwa sasa wapo nyuma ya Real Madrid na AC Milan pekee katika orodha ya timu ambazo zimetia kapuni mataji ya UEFA mara nyingi zaidi.

Tofauti nyingine kati ya fainali ya UEFA msimu jana na muhula huu, ni uwepo wa kipa Becker katikati ya michuma ya Liverpool ambao msimu uliopita walijipata wakiadhibiwa vikali na Real kwa hatua ya kumchezesha Lloris Karius aliyezidiwa maarifa na Karim Benzema na Gareth Bale jijini Kiev.

Alisson aliyesajiliwa kutoka AS Roma mwishoni mwa msimu jana, aliwadhihirishia wakosoaji wake kiini cha Liverpool kuweka mezani zaidi ya Sh10 bilioni ili kujivunia huduma zake.

Alisson na beki Virgil van Dijk ni miongoni mwa wachezaji ambao ukubwa wa mchango wao kambini mwa Liverpool nusura uwavunie waajiri wao taji la kwanza la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kipindi cha miaka 29.

Kinaya ni kwamba Liverpool walitawazwa mabingwa wa UEFA msimu huu licha ya kuanza kampeni zenyewe kwa matao ya chini. Licha ya kupoteza mchuano mmoja pekee katika kivumbi cha EPL, Liverpool walipigwa kumbo na Man-City katika dakika za mwisho na kuambulia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 98, moja pekee mbele ya kikosi cha Klopp.

Katika safari yao ya kufuzu, Liverpool waliwabwaga PSG 3-2 katika mkondo wa kwanza wa mechi ya makundi kabla ya kupepetwa 2-1 katika marudiano.

Baadaye walipokezwa kichapo cha 1-0 na Napoli ugenini kabla ya wao pia kusajili ushindi sawa na huo katika marudiano yaliyoandaliwa uwanjani Anfield. Liverpool baadaye waliwakomoa Crvena Zvezda 4-0 nao pia wakakung’utwa 2-0 katika mkondo wa pili.

Matokeo hayo yaliwaweka Liverpool katika nafasi ya pili kwenye Kundi C nyuma ya PSG. Ufufuo wao mwishoni mwa mechi za makundi uliwashuhudia wakiwabandua Bayern Munich kwenye hatua ya 16-bora kabla ya kuwadengua FC Porto kwenye robo-fainali.

Baadaye, walihitaji miujiza iliyowatoa nyuma kwa mabao 3-0 na hivyo kuwalaza Barcelona 4-0 katika marudiano ugani Anfield.

You can share this post!

Mane kushinda UEFA kwaipa Senegal motisha kufukuzia taji la...

Wanafunzi wahamasishwa kuhusu upandaji miti

adminleo